Rais Kikwete Amlilia Marehemu Jackson Makweta

Rais Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Rais Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na kuhuzunishwa na kifo cha aliyekuwa Mbunge mkongwe na Waziri wa miaka mingi katika Serikali za Awamu mbalimbali za uongozi wa Tanzania, Jackson Makweta ambacho kimetokea jioni Jumamosi, Novemba 17, 2012, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.

Katika salamu zake za rambirambi kwa familia ya Mzee Jackson Makwete, Rais Kikwete amemwelezea Mzee huyo kama mtumishi wa umma aliyejali sana ustawi wa jamii yake, mwanasiasa mkweli na mwadilifu, mbunge aliyeleta matumaini kwa aliowawakilisha na waziri aliyetoa mchango mkubwa katika Serikali alizozitumikia.

Rais Kikwete ameiambia familia hiyo ya Mzee Makweta: “Nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Mzee Jackson Makweta ambacho nimejulishwa kuwa kimetokea jioni ya leo. Kwa hakika Tanzania imempoteza mtumishi wa umma wa mfano na aliyejali sana ustawi wa jamii yake na mwanasiasa mkweli na mwadilifu.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Tutaendelea kumkumbuka Mzee Makweta kama mbunge ambaye alileta matumaini na kuongoza jitihada za wananchi wa Njombe Kaskazini kujiletea maendeleo na Waziri ambaye alitoa mchango mkubwa katika Serikali za Awamu mbali mbali za uongozi wa nchi yetu. Alikuwa kisima cha busara na mzoefu wa uongozi na ameondoka wakati bado tunahitaji sana uongozi na busara zake.”

“Nawatumieni nyinyi wanafamilia salamu zangu za rambirambi kwa kuondokewa na kiongozi na mhimili wa familia. Naelewa machungu yenu katika kipindi hiki. Naungana nanyi katika msiba mkubwa na majonzi mengi. Namwomba Mwenyeji Mungu, Mwingi wa Rehema, awape subira na uvumilivu ili muweze kuvuka kipindi hiki kigumu. Aidha, naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi pema roho ya Marehemu Jackson Makwete. Amina.”

Jiunge nasi kwenye social media
Facebook
Instagram
Youtube
Twitter

About The Author

Joachim Ernest Mushi, Kitaaluma ni mwanahabari muhitimu (Uandishi-2006) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC) kwa sasa Shule Kuu ya Uandishi na Mawasiliano. Nimekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi (Gazeti la Kulikoni & Thisday), Mwandishi mwandamizi Gazeti kongwe la Kiongozi, Mhariri wa Makala mwanzilishi wa Gazeti la Jambo Leo. Kwa sasa ni Mhariri Mkuu Kiongozi wa Thehabari.com, nchini Tanzania.

Related posts

Leave a Reply

Your email address will not be published.