Bolt na Rudisha waendelea kutesa Olimpiki

Mwanariadha maarufu nchini Kenya na duniani, David Rudisha
Mwanariadha maarufu nchini Kenya na duniani, David Rudisha

MKIMBIAJI wa kasi duniani kwa sasa ni Usain Bolt ambaye ametimka mbio na kufanikiwa kutetea taji lake la mbio za mita 200 katika michezo ya Olimpiki akiongeza mavuno ya nchi yake Jamaica ya medali za dhahabu.

Usain Bolt amekuwa pia mtu wa kwanza duniani kuweza kushinda mbio za mita 100 na 200 katika msimu mmoja wa Olimpiki. Lakini la kusisimua zaidi ni pale David Rudisha wa Kenya alipovunja rekodi ya dunia katika mbio za mita 800.

Mbio hizo zimefikisha kilele siku ya kihistoria wakati David Rudisha wa Kenya alipovunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 800, akiwaacha wakimbiaji wenzake nyuma mara tu baada ya mbio hizo kuanza.

Rudisha alikuwa akilenga kuweka historia tangu pale mbio hizo zilipoanza, akiwa mtu wa kwanza kukimbia mbio hizo chini ya dakika moja na sekunde 41. “Sikuwa na shaka yoyote na ushindi, lakini nilikuwa nasubiri mazingira maalum kuweza kuvunja rekodi hii, alisema Rudisha kwa kujiamini”.

Nae mkuu wa kamati ya maandaandalizi ya michezo hiyo ya London Sebastian Coe ambaye binafsi alikuwa akishikilia rekodi ya dunia ya mbio hizo za mita 800, amesema na hapa namnukuu: “Badala ya kufanya juhudi tu za kushinda, alitaka kufanya kitu cha ziada .. ..ushindi wa Rudisha utaingia katika historia kuwa ni mmoja kati ya ushindi adhimu katika Olimpiki”.

Kwa upande wake Usain Bolt muda aliotumia unafikisha muda wa nne kwa kasi katika mbio hizo wakati alipopunguza kasi katika mita 30 za mwisho, akihisi kuwa hajaweza kufikia nafasi ya kuweza kuvunja rekodi ya dunia. Medali ya fedha imekwenda kwa hasimu wake Mjamaica Yohan Blake na pia shaba ikaangukia huko huko Jamaica kwa Warren Weir. Nilijua kuwa itakuwa rekodi ya dunia nilipofika katika kona , nilikuwa nahisi hivyo, Bolt amesema. Nilitaka kwa dhati kujaribu kupata rekodi ya dunia katika mbio za mita 200 lakini ilikuwa vigumu kuliko nilivyofikiria.

Hata hivyo vumbi litatimka tena leo katika mbio za mita 100 wanaume kupokezana vijiti katika kuwania kufuzu katika fainali za mbio hizo. Oscar Pistorius wa Afrika kusini mwanariadha ambaye anatumia miguu ya bandia amenyimwa nafasi ya kushiriki mbio hizo. Pia kutakuwa na michuano ya awali ya mbio za mita 400 kupokezana vijiti kwa wanawake. Pia kutakuwa na fainali ya mbio za mita 1,500 kwa wanawake, pamoja na mbio za mita 5,000 wanawake.

Naye mwanariadha wa Ufaransa Hassan Hirt anayekimbia mbio za mita 5,000 amepigwa marufuku kushiriki katika mbio hizo baada ya kupatikana na hatia ya kutumia madawa ya kuongeza nguvu.

-DW

Jiunge nasi kwenye social media
Facebook
Instagram
Youtube
Twitter

About The Author

Joachim Ernest Mushi, Kitaaluma ni mwanahabari muhitimu (Uandishi-2006) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC) kwa sasa Shule Kuu ya Uandishi na Mawasiliano. Nimekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi (Gazeti la Kulikoni & Thisday), Mwandishi mwandamizi Gazeti kongwe la Kiongozi, Mhariri wa Makala mwanzilishi wa Gazeti la Jambo Leo. Kwa sasa ni Mhariri Mkuu Kiongozi wa Thehabari.com, nchini Tanzania.

Related posts

Leave a Reply

Your email address will not be published.