Askari wa Bunge wakiwasindikiza wabunge wa CHADEMA Tundu Lissu (kulia) , Mchungaji Peter Msigwa (kushoto) na Godbless Lema (wa pili kushoto) kuondoka nje ya viwanja vya Bunge mara baada ya Naibu Spika, Job Ndugai (hayupo pichani) kuwaamuru watoke ndani ya Bunge kwa kile kudai wamevunja kanuni za Bunge. Wa pili kulia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika akiwasindikiza.
Dodoma.
WABUNGE watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema (Arusha Mjini), Tundu Lissu (Singida Mashariki) na Mchungaji Peter Msigwa Mbunge wa Iringa Mjini jana wamefukuzwa bungeni.
Job Ndugai (Mbunge wa Kongwa) na Naibu Spika alitoa uamuzi huo mjini hapa majira ya saa 6 mchana ikiwa ni muda mfupi baada ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Lema, kusoma taarifa mbadala ya bajeti ya wizara hiyo.
Wakati Lema akiendelea, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, aliomba utaratibu kwa Naibu Spika kwa kile kutoridhishwa na kauli za Lema kwenye hotuba yake.
Lukuvi alisema; licha ya kwamba kila chama kina uhuru wa kueleza mtazamo juu ya wizara husika, lakini kinachowasilishwa na Lema hakikubaliki kwani hotuba yake imejaa maneno ya uchochezi.
Lukuvi alisema hata kanuni za bunge haziruhusu wabunge kuzungumza mambo wasiyokuwa na uhakika nayo. “Kuhusu utaratibu Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima zote za kiti chako na kwa maelekezo ambayo umekuwa ukitoa bungeni, Kanuni ya 64 imevunjwa na Mheshimiwa Lema wakati akiwasilisha hotuba yake hapa.
“Kanuni hii leo imevunjwa na hotuba nzima, kama ulivyotutangazia asubuhi, sisi tumekuwa wavumilivu sana, lakini Watanzania wenyewe watapima na kwa uvumilivu tulionao tulitaka yote yasikike ili Watanzania wenyewe wapime.
“Hivi Mheshimiwa Naibu Spika, mbunge aliyechaguliwa na wapiga kura anaweza kusema vile!, kuna maneno hapa yametumika kama Tanzania siyo nchi ya haki na heri kuwa na vita,” alisema Lukuvi.
Hata hivyo akiendelea zilianza kelele kutoka upande walikokaa wabunge wa CHADEMA, hivyo Naibu Spika kuingilia na kumpa nafasi Lukuvi kuendelea kueleza. “Polisi leo wanaagizwa wakiuke maagizo ya makamanda wao na hata kama kuna maandamano wasiende kuyalinda, tunaambiwa uchaguzi wa Arusha ni batili, kwa kweli hotuba hii ya Lema imejaa uchochezi mkubwa, yaani kuanzia mwanzo mpaka mwisho wake…
Baadaye Lissu alisimama kuomba mwongozo; “hivi huyu ameomba utaratibu au anatoa hotuba?”. Lissu alipokuwa akiendelea, Lema akasimama na kuomba naye mwongozo. Kabla hajazungumza, Naibu Spika akasimama, Mchungaji Msigwa naye akasimama na kusema; “huu ni upendeleo wa hali ya juu, huyu amesimama kuomba utaratibu na sasa anahutubia, maana yake nini?”.
Ndipo Naibu Spika akasimama na kuendelea; “Kwa kuwa nimesema tangu asubuhi kwamba hakuna kuzungumza bila ruhusa…kuna watu watatu nimewaona wakizungumza bila kufuata utaratibu, sasa watu hao watatolewa nje ya Bunge sasa hivi.
“Mtu wa kwanza ni Tundu Lissu, mtu wa pili ni Mchungaji Msigwa na wa tatu ni Lema, nawaomba watoke nje sasa hivi na nitahakikisha wanasindikizwa hadi nje ya geti la Bunge kabisa,” alisema Naibu Spika na wabunge hao kuondolewa bungeni.
Mimi kwa maoni yangu baadhi ya wabunge na hasa wa Chadema wanaonesha kukosa maadili na ustaarabu mbunge anaotarajiwa kuwa nao. Nawakumbusha kwamba kazi ya msingi kabisa ya wabunge ni kutunga sheria. Heshima ya bunge na wabunge inategemea sana kuheshimiwa kwa sheria. Maana kama sheria hazitakuwa zinaaminiwa na kuheshimiwa wabunge watakuwa hawana maana yoyote katika jamii. Inatia simanzi kuona wabunge ambao wanaheshimika kwaajili ya sheria kuheshimika wanakuwa wa kwanza kudharau na kuvunja sheria.
Kwa mujibu wa sheria na kanunu za bunge, vikao vya bunge vinaendeshwa na spika au mwenyekiti. Mwenyekiti au spika anapoongoza bunge ni lazima aheshimiwe. Sasa hawa ndugu zetu unakuta spika anamuelekeza asiongee bila ruhusa yake anaendelea kuongea na tena kujibizana kwa kejeri. Watoto wa shule za msingi wanaoangalia vipindi vya bunge wanajifunza nini?
Unakuta mbunge anatumia muda mrefu kujisifu na kusifu chama chake huku akitumia lugha ya kejeri, maudhi na wakati mwingine matusi katika kujenga au kusisitiza hoja yake. Kwa msingi huu watu tunashindwa mara nyingine kutofautisha mijadala ya masuala mhimu bungeni na ile tunayofanya kila siku kwenye vijiwe vyetu vya kahawa. Maana lugha na staili zinazotumika kujadiliana sasa hivi bungeni hazipishani sana na mara nyingine zinazidiwa na zile za vigenge vya mikahawani.
Nionavyo mimi hoja inaeleweka na kupokeleka zaidi ikiletwa katika lugha yenye heshima. Ni mara ngapi hoja zikitolewa na wapinzani kwa lugha ya heshima zinapokelewa na kuungwa mkono na wabunge wa CCM?
Kwa upande mwingine pia ni mhimu kuzingatia kwamba mbunge ni binaadamu na mtanzania kama wengine. Licha ya mamlaka yake makubwa ya kibunge bado anatarajiwa kuishi katika maadili ya kitanzania. Ndio mbunge mwenye miaka 30 kisheria ana hadhi na haki sana na yule wa miaka 70. Ana uhuru wa kutoa hoja inayopingana naye kwa uwazi. Lakini hilo haliondoi wajibu wa kijamii kwa mbunge huyu kijana kumpa heshima yake mbunge mzima. Kusema kwamba Waziri Mkuu amekosea ama amepitiwa katika majibu yake kisemantiki inaweza kuwa na maana sawa kwamba majibu ya Waziri Mkuu siyo ya kweli. Ki staili na maadili ya lugha maneno hayo yana maana tofauti kabisa. Sembuse kumuambia ni muongo.
Ningewaomba wabunge tujitahidi kuwa na heshima, adabu na maadili wakati tunatimiza wajibu wetu wa kuwatumikia wananchi.
George, ni dhahiri kwamba demokrasia ya nchi yetu sasa inakuwa. Binafsi nimefarijika sana kuona idadi ya wabunge pinzani wameongezeka na wanaihoji Serikali vilivyo. Tatizo linaloendelea Bungeni sasa ni kwamba kanuni nyingi za Bunge zimepitwa na wakati na zinatakiwa zibadidilishwe ili kuendeana na maudhui ya Bunge la sasa. Nchi yetu haina tena mfumo wa chama kimoja!
Kwa mfano, moja ya Kanuni za uendeshaki wa shughuli za bunge inasema “Spika ataongoza kila Kikao cha Bunge na ndiye mwenye mamlaka ya kuamua mambo yanayoweza kuzungumzwa Bungeni.” Hii kanuni haifai katika mazingira ya vyama vingi, kwani Spika kama binaadam anaweza akapendelea kwa kukipa nafasi chama chake tu kuzungumza yale yanayokipendeza chama na serikali yake. Mzee Samuel Sitta alijitahidi sana katika hili, kwani alikuwa anatoa fursa sawa kwa wabunge wote kutoa hoja zao kama tulivyoshuhudia kwenye bunge lililopita. Matokeo yake Mzee Sitta aliwekewa zengwe na CCM, na leo hii si spika tena.
Mh. Makinda ameshaonyesha usdhaifu mkubwa katika kusimamia kanuni hii na bunge kwa ujumla. Kwa maana hiyo basi, wabunge wa upinzani wakati mwingine wamekuwa wakikaidi kunyamanzishwa pindi wanapotaka kuzungumzia matatizo ya wanachi wao. Lengo langu sio kusema kwamba wabunge wapewe fursa ya kuzungumza lolote wanalotaka Bungeni, bali nataka wabunge wapewe ruksa ya kuzungumza lolote linalohusiana na kero za wanachi wa maeneo yao na Tanzania nzima kwa ujumla. Muda ule wa “adabu za uwoga” wa chama kimoja umeshapitwa na wakati.
Poel ni kweli demokrasia imekuwa. Yawezekana pia kuna mapungufu kwa upande wa spika katka kuzitumia vizuri kanuni za bunge. Hoja yangu kubwa ni kwamba hata kama kuna matatizo kama hayo, wabunge wa upinzani na wengine wanaobaini hayo mapungufu watumie lugha za kistaarabu katika kujenga hoja zao na kuibua mapungufu. Spika akielezwa kwa lugha nzuri mapungufu yake akayaelewa naamini atazingatia. Na hata wabunge wengine wakiyaona na kuyaelewa mapungufu yake watakuwa ni msaada katika kufikisha ujumbe kwa spika