Tume ya Kuchunguza Kufeli kwa Kidato cha Nne 2012 Yaomba Maoni kwa Wadau

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya kuchunguza kushuka kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne 2012, Prof. Sifuni Mchome (katikati) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu kuanza kwa zoezi la ukusanyaji wa maoni kutoka wadau mbalimbali. Wengine ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene (kushoto) na Bi. Tunu Temu mjumbe wa Sekretarieti ya Tume hiyo.

Picha/Habari Na Aron Msigwa – MAELEZO, Dar es Salaam

TUME ya Taifa iliyoundwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuchunguza kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa Wanafunzi wa Kidato cha Nne Mwaka 2012 imewaomba Watanzania kuipa ushirikiano kwa kutoa maoni yao ili iweze kukamilisha majukumu iliyopewa kwa muda na ufanisi mkubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa Tume hiyo Prof. Sifuni Mchome ameeleza kuwa tume hiyo ilianza kazi mara baada ya kuzinduliwa na Waziri mkuu tarehe 2 mwezi Machi mwaka huu na kufafanua kuwa jukumu lililopo sasa ni kuanza kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa watanzania ili kubaini sababu za matokeo mabaya ya mtihani huo.

Amesema kuwa tume hiyo pamoja na mambo mengine imepewa jukumu la kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua ili kukabiliana na tatizo la mwenendo wa kushuka kwa kiwango cha elimu nchini huku mapendekezo hayo yakizingatia kipindi cha muda mfupi, kati na kipindi cha muda mrefu.

Prof. Sifuni ameeleza kuwa tume hiyo inafanya kazi kwa kuzingatia hadidu mbalimbali za rejea zikiwemo kubainisha sababu za matokeo mabaya ya kidato cha nne 2012, sababu za kushuka kwa kiwango cha ufaulu, nafasi ya Halmashauri katika kusimamia elimu ya sekondari katika halmashauri zake.

Rejea nyingine ni pamoja na pamoja na kuanisha sababu nyingine zinazoweza kuwa zimechangia hali ya matokeo hayo pamoja na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua mara moja kwa wanafunzi 240,903 waliofeli mitihani yao kwa kupata daraja sifuri.

Amefafanua kuwa tume katika kutekeleza majukumu yake itapitia mitaala na mihutasari ya Elimu ya Msingi na Sekondari, kutathimini kiwango na mazingira ya ufundishaji na ufunzaji, kuangalia mfumo wa upimaji na tathmini ya mitihani pia usimamizi na uendeshaji.

Pia pamoja na mambo mengine tume itatathmini mchango wa jamii na wazazi/ walezi katika maendeleo ya wanafunzi, hali ya upatikanaji wa chakula cha mchana, upungufu wa majengo ya shule,madarasa, maabara na maktaba.

Vilelevile tume hiyo itafuatilia mwamko wa wazazi katika kufuatilia mkazo wa eliimu kwa watoto na suala la mmomonyoko wa maadili unaotokana na ukuaji wa utandawazi hususan teknolojia ya Habari na Mawasiliano na kutathmini athari ya mfumo wa ufundishaji wa mikondo miwili iliyopo katika shule za Zanzibar.

Aidha mwenyekiti wa Tume hiyo amebainisha kuwa tume itaanza rasmi kukutana na wadau mbalimbali kwa lengo la kupata maoni kuanzia tarehe 11 mwezi huu kwa kuanza na mkoa wa Dar es salaam, Zanzbar na maeneo mengine nchini kwa kukutana na viongozi wa ngazi mbalimbali za Wizara, Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Kata, Shule, Taasisi mbalimbali za kijamii na wananchi kwa ujumla na pia kuwasilisha maoni kwenye tume kupitia Mwenyekiti wa Tume, Tume K4-2012, S.L.P 5909 Dar es salaam au kupitia simu 0737206038, Barua pepe: maoni@tumek4.go.tz au kwa kutembelea Tovuti ya tume ya www.tumek4.go.tz.

Related Post

One thought on “Tume ya Kuchunguza Kufeli kwa Kidato cha Nne 2012 Yaomba Maoni kwa Wadau

  1. TUWALAUMU WASOMI WA TANZANIA AMBAO WALINYAMAZA WAKATI SERIKALI IKIFANYA MAAMUZI MEPESI YATAKAYOSABISHA ATHARI KUBWA KWA KIZAZI CHA LEO NA KIJACHO BAADHI YA MAAMUZI HAYO MEPESI WAKIFIKIRI WANAPUNGUZA GHARAMA NI ;01: KUONDOA AZIMIO LA ARUSHA LILILOKUWA NA SERA YA ELIMU JE SERA YA ELIMU YA AZIMIO LA ZANZIBAR NI IPI? 02: KUONDOA JKT LILILOWAJENGEA UTAMADUNI WA AINA MOJA WATANZANIA WOTE LEO WAALIMU WAMEKOSA UZALENDO WAPO WAALIMU PAY ROLL,WAALIMU WATAZAMAJI WENYE UELEWA FINYU WA MAADILI YA UALIMU WA[INDUCTION COURSE] 03:KUFUTA MITIHANI YA MCHUJO YA DARASA LA NNE ILI KUPUNGUZA GHARAMA LEO VIJANA WENGI WANAMALIZA DARASA LA SABA BILA KUJUA KUSOMA NA KUANDIKA NA KUHESABU 04:KUFUTA MITIHANI YA FORM TWO LENGO KUONGEZA WATAALAMU /WAKATI WAKIHOFIA GHARAMA ZA MITIHANI LEO IDADI KUBWA YA WANAOHITIMU KIDATO CHA NNE NI DIVISHENI “O” NA “IV” 05:KUCHAGUA WANAFUNZI WASIO NA UWEZO NA WASIO NA MAADILI YA UALIMU KUSOMEA UALIMU KAZI AMBAYO AWALI ILIFIKIRIWA NI KAZI TAKATIFU [UALIMU SIO WITO TENA NI AJIRA KAMA AJIRA NYINGINE] PESA KWANZA WITO BAADAYE 06: KUTUMIA UWANJA MMOJA TU “COGNITIVE” KUWA KIGEZO CHA UFAULU WA WANAFUNZI WAKATI NYANJA ZINGINE KAMA “AFFECTIVE” INAYOHUSU MAADILI YA MWANAFUNZI NA”PSYCHOMOTOR” SHUGHULI ZINAZOHUSU MATUMIZI YA MISULI KATIKA UTENDAJI HAZIPIMWI KWENYE MITIHANI YA MWISHO HALI INAYOFANYA WATAHINIWA WENGI WANAOMALIZA WASIPOKUWA NA SIFA ZA KUAJIRIWA “WHITE COLLAR JOBS” WANAJIONA WAMESHINDWA KATIKA MAISHA NDIO WALIOJAZANA KWENYE VITUO VYA MAGARI KAMA WAPIGA DEBE,NYOKA KWENYE MIGODI YA MADINI KWANINI WAMMETAHINIWA KWENYE SILABUS “CONTENT BASED”WAKATI KWENYE FIELD SILABUS INAYOTAKIWA NI”CONTENT COMPETENCE BASED” WATANZANIA TUFIKIE MAHALI WOTE KWA UJUMLA WETU TUJILAUMU KWA KUWA NA WATOTO WENYE NIDHAMU MBAYA WASIOSHAURIKA WASIOONYEKA WASIOFUNDISHIKA KUTOKANA NA KUUVAMIA UTANDAWAZI BILA KUUCHUJA WAKALA WA MALEZI YA VIJANA WAMEKUWA CHACHU YA MMOMONYOKO WA MAADILI WAKALA HAO NI WAZAZI, JAMII, SHULE, TAASISI ZA DINI, VYOMBO VYA HABARI NA MAWASILIANO, MAKUNDI RIKA NA SERIKALI WOTE HAWA WAMEKUWA “SPONJI”KUNYONYA UCHAFU WOTE WA UTANDAWAZI NA KURITHISHA KIZAZI CHA LEO NA KESHO KISICHOAMBILIKA ,KISICHOJUA KUNA BABA AU MAMA ,KINACHOJISIFU,RAHISI KUSHAURIKA KUVUNJASHERIA KIKICHUKUA SHERIA MIKONONI ,MATUSI,WAVIVU WA KUFIKIRI KUTATA MAFANIKIO YA HARAKA AKILIMA ASUBUHI ANATAKA AVUNE JIONI WANA DHARAU KUBWA KWA WAZEE WAO

Comments are closed.