Halmashauri Zashauriwa Kubuni Vyanzo vya Mapato

mama aliyejitwisha Mkungu wa ndizi akipeleka sokoni

Na Immaculate Makilika- Dodoma

SERIKALI inatambua kazi kubwa zinazofanywa na wenyeviti wa vijiji na vitongoji katika kuhimiza na kusimamia shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao. Serikali inapeleka rasilimali fedha, vifaa na rasilimali watu kwa wingi katika mamlaka ya Serikali za Mitaa.Uamuzi huu wa Serikali umesaidia kuwapa fursa wananchi kujiwekea vipaumbele vya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia fursa na vikwazo vilivyopo.

“Viongozi hawa wana majukumu ya kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika uchangiaji wa miradi ya Maendeleo na kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kupitia kamati za maendeleo za vijiji “alisema Naibu Waziri wa Fedha Janet Mbene kwa niaba ya Waziri Mkuu.

Aidha Naibu huyo aliendelea kwa kusema kwamba, kwa kutambua uzito wa majukumu haya, Serikali kupitia kila Halmashauri imeweka utaratibu wa kuwalipa posho wenyeviti wa vijiji na Mitaa kutokana na vyanzo vya mapato ya ndani ambayo ni asilimia 20 ambapo kati ya hizo asilimia 3 ni fedha za maendeleo na asilimia 17 ni kwa ajili ya ya shughuli za utawala ikiwemo kulipa posho.

Hata hivyo, viwango ambavyo hulipwa vinatofautiana kati ya halmashauri moja na nyingine kulingana na uwezo wa kukusanya mapato ya ndani katika vyanzo vilivyopo. Aidha changamoto kubwa inayoikabili ni ufinyu wa bajeti pamoja na makusanyo kidogo katika halmashauri

Aidha, mkazo umekua ukitolewa kwa halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa asilimia 20 ya mapato ya ndani ya halmashauri zinapelekwa katika vijiji,kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kubuni vyanzo vipya vya mapato.