Al Shaabab Wavamia Msikiti Kenya, Auwawa kwa Risasi Burundi

Baadhi ya wapiganaji wa Al Shaabab.

Baadhi ya wapiganaji wa Al Shaabab.


VIONGOZI Kaskazini mwa Kenya wamesema wapiganaji wa kundi la kigaidi kutoka Somalia la Al Shaabab wamevamia msikiti mmoja eneo la Garissa kwa masaa kadhaa. Wapiganaji hao waliwahutubia waumini waliokuwa msikitini kwa karibu saa mbili kabla ya kutokomea msituni.

Katika hotuba yao waliikosoa serikali ya Kenya na kuonya waumini dhidi ya kuwa majasusi wa serikali ya Kenya. Mwezi uliopita Al Shaabab walivamia chuo kikuu cha Garissa na kuwaua watu 150 wengi wao wakiwa wanafunzi. Kundi hilo kutoka Somalia linaaminika kuwa na wafuasi nchini Kenya ambapo limetekeleza mashambulizi kadha katika jitihada ya kuilazimisha serikali ya Kenya kuondoa majeshi yake nchini Somalia.

Majeshi ya Kenya ni miongoni mwa kikosi cha kulinda amani cha muungano wa Afrika Amisom ambao wanaisaidia serikali dhaifu ya Somalia kupigana na waasi wa Al Shabaab. Msikiti huo upo takriban kilomita 40km kutoka Mji wa Garissa kulikotokea shambulizi la chuo kikuu mwezi uliopita.

Walioshuhudia wanasema kuwa wapiganaji hao walikuwa wameandamana na wapiganaji takriban 40 waliojihami tayari kwa vita. BBC mjini Nairobi ilisema kuwa serikali ya Kenya imeanza kujenga ua ilikuzuia mashambulizi kama hayo.

Wakati huo huo, habari kutoka Burundi zinasema kuwa mtu mmoja amepigwa risasi na kuuawa katika mji mkuu wa Bujumbura. Mtu huyo alikuwa miongoni mwa waandamanaji wanaopinga hatua ya rais Pierre Nkurunziza kugombea urais kwa awamu ya tatu.

Walioshuhudia wanasema kuwa polisi walimpiga mwandamanaji huyo risasi mgongoni wakiwa katika eneo la Musaga linalotazamwa kama ngome ya upinzani. Waandamanaji walijaribu kufika katikati mwa jiji la Bujumbura lakini walitimuliwa kwa mabomu ya moshi wa kutoa machozi.

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, amewaomba zaidi ya raia laki moja na hamsini waliokimbia ghasia nchini humo katika majuma kadhaa yaliyopita, warejee nyumbani. Katika hotuba kwenye runinga ya taifa, amesema kuwa asilimia tisini na tisa nukta tisa ya Burundi ina amani. Anasema kuwa hakuna mtu yeyote anayetaka kufufua taharuki ya kikabila.

Rais Nkurunziza amewataka raia wa Burundi waliotoroka warejee nyumbani kwani kuna amani Muda mchache baadaye rais Nkurunziza alionekana akicheza mpira na maswahiba wake wa karibu licha ya maaandamano yanayoendelea mjini Bujumbura. Kumekuwa na hali ya taharuki mjini Bujumbura haswa kutokea jumatano iliyopita baada ya jaribio la mapinduzi dhidi ya rais Nkurunziza.
-BBC