Dk Nchimbi atoa siku 75 kusakwa vazi la taifa

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi (wa kwanza kushoto) akizindua Kamati ya kukamilisha mchakato wa kupata Vazi la Taifa, wa pili kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Sihaba Nkinga na wengine ni Wanakamati wa zoezi hilo .Shughuli hiyo ilifanyika kwenye Ukumbi wa Miundombinu jijini Dar es Salaam leo. Picha na Anna Itenda – Maelezo.

Na Beatrice Mlyansi na Benjamin Sawe

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi ameitaka kamati mpya ya kubuni vazi la taifa kukamilisha mchakato wa kupata vazi hilo ndani siku 75 ili liweze kupelekwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa uamuzi zaidi.

Akizungumza na wanahabari Jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa kamati hiyo, Waziri Nchimbi amesema kazi ya kamati hiyo siyo kuanza mchakato upya bali ni kukamilisha mchakato wa kupata vazi la taifa la mwanaume na mwanamke ulioanza tangu mwaka 2004.

Amesema Wizara imefanya mambo kadha wa kadha katika kukamilisha zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kutembelea nchi kadhaa za Afrika ili kupata uzoefu wa namna walivyopata vazi la taifa. Amesema anaamini kwa kupitia mapendekezo ya awali ya kamati na taaluma yatasaidia mchakato huo ili kuwe na vazi la taifa.

“Mnayo kazi kubwa kwa sababu lazima tufike mwisho tuwape Watanzania kile ambacho wamekisubiri kwa muda mrefu, Watanzania wanatarajia ufanisi mkubwa kutoka kwa kamati hii.” Alisema Waziri Nchimbi. Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo, Joseph Kusaga amesama watajitahidi kufanya kazi kwa nguvu zote kuhakikisha nchi inapata vazi la taifa kwa sababu ni kitu kizuri nchi kuwa na vazi lake.

Hivi Karibuni Waziri Nchimbi aliteua wajumbe wa kamati maalum inayoongozwa na Joseph Kusaga ambaye ni Mweneykiti ili kufankisha mchakato wa kupata vazi la taifa, wajumbe wengine walioteuliwa ni pamoja, Angela Ngowi Katibu, Joyce Mhavile, Mstafa Hassanali, Absalum Kibanda, Habibu Gunze, Makwaia Kuhenga na Ndesambuka Merinyo.

Wakati huo huo Waziri ametoa pole kwa Watanzania wote waliokumbwa na mafuriko yaliyosababisha kupoteza maisha kwa baadhi ya watu na mali kuharibiwa, pia amewapongeza wanahabari kwa kuhabarisha umma licha ya kufanya kazi katika mazingira magumu.

Related Post

4 thoughts on “Dk Nchimbi atoa siku 75 kusakwa vazi la taifa

  1. Huu si kama ujinga ni nini? Hivi Dr. kweli na akili zake timamu anataka kutulazimisha kuvaa nguo za ajabu? Nani anajali vazi la taifa, hii ni karne ya 21 na tunazidi kwenda mbele vazi la taifa litatuletea maendeleo gani? Nchi haina umeme, maji, barabara mbovu kila pande ya nchi, badala ya kuhangaikia masuala nyeti ya nchi yetu mnataka kutuletea upuuzi wa vazi la taifa. Watu kibao wamepatwa na maafa ya mafuriko hapa Dar, kwa nini msikae na kujadili haya? Upuuzi huu, hivi huyu ni Dr. kweli ama ni wale wale vihiyo?

  2. Nimeona juhudi kubwa sana katika hili la vazi la taifa ambazo kwa kutaka kufanana na wengine si mbaya.
    Lakini hebu turejee nyuma kidogo tukumbuke kuwa sisi japo hatukujaliwa vazi kama vile ndugu zetu wa Nigeria, Ghana, South Africa na kwingineko sisi tuna jambo ambalo wenzetu wanatuonea gele tena lenye manufaa ya wazi zaidi kuliko vazi nalo ni LUGHA YA TAIFA. Jaribu kuwaza nchi kama Uswisi hawana lugha ya taifa sisi tunayo, Nigeria pamoja na utajiri mkubwa wa mafuta na wingi wa vyuo vikuu lakini kitovu kimojawapo cha machafuko walioyo nayo ni tofauti zao za kikabila ambazo kila kukicha zinazidi kuwagawa. Ukimuuliza Mnigeria ye yote aliyefika Tanzania hatuoni kuwa hatuna cha kujivunia kwa kukosa vazi la taifa bali anatuonea wivu kwamba po pote mtu aendapo Tanzania nzima ana uwezo wa kuwasiliana na mtu mwingine si kwa kiingereza wala lugha nyingine ila kiswahili. Wanatushangaa sana kwamba tumewezaje kufikia kiwango hiki na wangetamani na wao kuwa na lugha ya taifa ambayo si kiingereza ambacho si chao. Sasa sisi wenye nacho kitu ambacho ni chanzo kikubwa cha amani na maelewano katika taifa letu tunadharau na kuona kana kwamba ingekuwa kheri tuwe na vazi la taifa. Hebu tutazame njia za kukinadi zaidi kiswahili nje na kukitumia kwa ufasaha zaidi kuliko kumdharau Mungu ambaye ametupa hazina hii kubwa na kukosa shukurani kana kwamba hatuoni matokeo ya kuwa na lugha moja yenye manufaa zaidi kuliko kuwa na vazi moja. Jamani Mungu katupendelea sana sisi kwa kutupa lugha ya taifa na wala si vazi la taifa. tuna faida kubwa zaidi ambayo ni vema kuanza kuitumia sasa kuliko kushindana na watu ambao wamepewa kitu ambacho wala faida nacho kubwa hawana kuliko sisi.
    TUJUVUNIE KUWA NA LUGHA YA TAIFA TUWAACHE NA MAVAZI YAO YA TAIFA TUONE MWENYE FAIDA KUBWA ZAIDI NANI. Mbona Japan, Amerika, China Ujerumani wanatumia lugha ya kiswahili kujitangaza kwetu na si kutumia vazi la nchi nyingine kujionyesha mshikamano wao na nchi hizo?
    Kiswahili tukiboreshe tujivunie tulichonacho

    1. Asante sana Chriss kwa maoni yako, lakini ninaombi moja naomba nitumie maoni yako kuyachapisha kama uchambuzi ili yaweze kusomwa zaidi na wasomaji wetu. Asante na endelea kuwa mdau wa Mtandao wa dev.kisakuzi.com. Mhariri.

Comments are closed.