Zitto aeleza kwanini Tanzania hainufaiki kwa madini, Prof Shivji ahoji kauli za kukua kwa uchuni!

Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere-UDSM, Prof. Issa Shivji.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere-UDSM, Prof. Issa Shivji.

Na Joachim Mushi

NAIBU Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Kabwe Zitto amesema ni vigumu Tanzania kuanza kunufaika na sekta ya madini kama itashindwa kushinikiza kuanza kutumika kwa sheria mpya ya uchimbaji madini nchini.

Amesema kutoanza kutumika kwa sekta hiyo kumeigharimu nchi kiasi kikubwa, kutokana na mapato mengi ikiwemo malipo ya mrahaba katika kampuni anuai za madini.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akichangia mada zilizowasilishwa na wawezeshaji kutoka Kogoda cha Taaluma ya Mwalimu Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwenye tamasha la Kumi la Jinsia linaloendelea viwanja vya TGNP.

Mmoja wa wafanyakazi kutoka Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Sabato Nyamsenda (kushoto) akisikiliza kwa makini michango ya washiriki wa mada mara baada ya kuwasilisha mada yake iliyokuwa ikisema 'Uwekezaji katika sekta ya Madini Unamnufaisha nani?' (Picha zote na Joachim Mushi)

Amesema madini yanayochimbwa nchini yamekuwa yakisafirishwa kama yalivyo kitendo ambacho kimekuwa kikilisababishia Taifa kupoteza kiasi kikubwa cha mapato. Amesema kutokana na usimamizi mbovu hata bidhaa nyingi na malighafi zinazotumika kwenye makampuni ya madini zinatoka nje ya nchi.

“Hadi mwaka 2008, kati ya makampuni yote yanayochimba madini nchini ni mgodi mmoja tu (Bulyahulu) ndio ulikuwa ukitumia umeme wa Tanesco kuendesha shughuli zake, migodi mingine yote ilikuwa ikizalisha umeme wake. Na hata mafuta yanayotumika kuzalisha umeme zimekuwa zikiomba punguzo la kodi katika uagizaji….” Hata fedha inayopatikana katika uuzaji wa madini nje imekuwa ikipatikana kama takwimu, haiingii katika benki zetu,” alisema Zitto.

Awali akiwasilisha mada katika mjadala huo, Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Issa Shivji alisema kuna maswali mengi ya kujiuliza Watanzania, dhidi ya kauli zinazotolewa na Serikali kuwa uchumi umekuwa- ilhali hali za wananchi wengi kimaisha ni duni.

“Kuna maswali mengi ya kujiuliza juu ya kauli za viongozi zinazoeleza kuwa uchumi wa Tanzania umekuwa. Je, uchumi umekuwa, na umasikini umeongezeka, wasio na kazi hawajapungua ukuaji uchumi unamnufaisha nani?

Kama uchumi umekuwa kwanini hali za maisha ya wananchi wengi zipo chini? Ajira imepanuka sawia na upanukaji uchumi?,” alisema katika mada yake Prof. shivji.

Jiunge nasi kwenye social media
Facebook
Instagram
Youtube
Twitter

About The Author

Joachim Ernest Mushi, Kitaaluma ni mwanahabari muhitimu (Uandishi-2006) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC) kwa sasa Shule Kuu ya Uandishi na Mawasiliano. Nimekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi (Gazeti la Kulikoni & Thisday), Mwandishi mwandamizi Gazeti kongwe la Kiongozi, Mhariri wa Makala mwanzilishi wa Gazeti la Jambo Leo. Kwa sasa ni Mhariri Mkuu Kiongozi wa Thehabari.com, nchini Tanzania.

Related posts

Leave a Reply

Your email address will not be published.