Wenye Ardhi Bonde la Kilombero Kusaidiwa Kuzalisha Mpunga – Kikwete

Baadhi ya wakulima wa mpunga wakifanya palizi katika shamba lao kwenye Bonde la Kilombero
Baadhi ya wakulima wa mpunga wakifanya palizi katika shamba lao kwenye Bonde la Kilombero

Na Mwandishi Maalumu, New York, Marekani

SERIKALI ya Tanzania imefanikiwa kuainisha (identify) kiasi cha hekta 100,000 za ardhi ya wakulima wadogo ambao watasaidiwa kuongeza uzalishaji wa mpunga ili kuiwezesha Tanzania kuzalisha kiasi cha tani milioni moja za mpunga katika mwaka mmoja katika hatua ya kwanza ya kuleta mageuzi ya kilimo nchini.
Zoezi hilo ni sehemu ya mipango ya Serikali kuainisha kiasi cha hekta 200,000 za wakulima wadogo ili wasaidiwe kuongeza uzalishaji wa mpunga katika maeneo mbali mbali nchini, na hasa katika Bonde la Mto Kilombero, chini ya mipango mbali mbali ya kukuza kilimo kwa haraka, kuongeza uzalishaji wa mazao mbali mbali na kuwatoa wananchi katika umasikini.
Hayo yameelezwa Oktoba 2, 2012, na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Misaada ya Kimataifa ya Maendeleo la Marekani (USAID), Rajiv Shah, katika Hoteli ya JW Marriott, mjini New York, Marekani ambako Rais Kikwete amefikia katika ziara yake ya siku mbili.
Rais Kikwete na Shah wamejadili mipango mbali mbali inayosaidiwa na USAID, washirika wengine wa maendeleo na makampuni binafsi ya kimataifa katika jitihada za Tanzania kukuza kilimo na kupunguza umasikini ukiwamo ule wa SACGOT, Grow Africa na New Alliance for Agriculture.
Rais Kikwete amemweleza Shah kuwa mkulima mdogo na ardhi yake, hata ni ndogo kiasi gani, ni muhimu na ni sehemu maalum ya mipango ya Serikali katika kuendeleza kilimo kwa kumwinua mkulima huyo mdogo kutoka kwenye umasikini kwa kumsaidia kuboresha kilimo chake na uzalishaji wake.
“Kwa hakika, mkulima mdogo ni kiungo muhimu sana katika jitihada zetu. Lazima tutamsaidia kumtoa kwenye umasikini kwa kuongeza thamani kwenye ardhi yake, hata kama ni ndogo kiasi gani. Wakipewa pembejeo na misaada mingine wanaweza kuonyesha maajabu,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete pia amemweleza Shah kuhusu mipango ya Serikali ya kuanzisha Soko la Mazao ambalo litakuwa mkombozi kwa mkulima wa Tanzania na pia kuunda chombo maalum cha kushughulikia mageuzi katika kilimo cha Tanzania.
Shah amemwahidi Rais Kikwete kuwa Serikali ya Marekani kupitia USAID itakuwa tayari kusaidia jitihada hizo za Serikali katika kuunda vyombo hivyo viwili ili kumsaidia mkulima na kilimo cha Tanzania.

Jiunge nasi kwenye social media
Facebook
Instagram
Youtube
Twitter

About The Author

Joachim Ernest Mushi, Kitaaluma ni mwanahabari muhitimu (Uandishi-2006) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC) kwa sasa Shule Kuu ya Uandishi na Mawasiliano. Nimekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi (Gazeti la Kulikoni & Thisday), Mwandishi mwandamizi Gazeti kongwe la Kiongozi, Mhariri wa Makala mwanzilishi wa Gazeti la Jambo Leo. Kwa sasa ni Mhariri Mkuu Kiongozi wa Thehabari.com, nchini Tanzania.

Related posts

Leave a Reply

Your email address will not be published.