Waziri Mkuu Ahaidi Kuchangia Ujenzi Kituo cha Afya, Awataka Wakulima Kula Nyama

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwa ziarani mkoani Katavi. (Picha na Chris Mfinanaga)
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwa ziarani mkoani Katavi. (Picha na Chris Mfinanaga)

Na Mwandishi Maalumu, Katavi

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameahidi kuchangia sh. milioni 20 za kuanzia ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Mwamapuli ili kiweze kusaidia kata za jirani za Mbede na Majimoto.

Alitoa ahadi hiyo Desemba 20, 2012 wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Mwamapuli kwenye mradi wa mashine ya kukoboa mpunga akiwa katika siku ya nane ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.

“Hapa Mwamapuli hatuhitaji tena kuzungumzia habari ya zahanati sababu mmezungukwa na vijiji vingi na kata nyingi. Mnahitaji kituo cha afya ili kata za jirani za Mbede na Majimoto ziweze kunufaika,” alisema.

Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Katavi aliwaambia wakazi hao kwamba wakimaliza kazi ya kuvuna, waweke mpango mahsusi wa kuchangia matofali kwa kila kaya, na kila kijiji ili kusaidia ujenzi wa kituo hicho.

Aliwasihi watendaji na wenyeviti wa vijiji wasiwabugudhi wananchi kuhusu michango hiyo hadi watakapomaliza msimu wa kilimo. “Tuwaache wamalize kuvuna ndipo wachangie, tunataka kituo hiki kiwe kimefunguliwa ifikapo mwaka 2015,” alisema huku akishangiliwa.

Pia aliwataka wafugaji na wakulima wakae kwa kuheshimiana. “Wafigaji lazima tuendelee kuheshimu wakulima, tusipeleke mifugo kwenye mashamba yao. Kuheshimiana ndiyo kutatuondolea balaa la kupigana,” alisisitiza.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Pinda amewataka wakulima wa kata ya Mwamapuli wakubaliane kula njama na wakatae kuuza mpunga kutoka bonde la Rukwa ili wanunuzi wote wanunue mchele badala ya mpunga.

Alitoa rai hiyo Desemba 20, 2012 wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Mwamapuli kwenye mradi wa mashine ya kukoboa mpunga akiwa katika siku ya nane ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.

Alisema kuuza mchele kutaongeza thamani ya zao hilo na hivyo kufanya bei iwe juu. “Itabidi diwani na viongozi wengine wakae na wananchi na kupanga bei ya kuuza mchele wao ili kuwa na sauti ya pamoja,” alisema.

Alisema mashine hiyo ya kukoboa ina uwezo wa kukoboa magunia 400 kwa siku kwa hiyo wana uhakika wa kusindika kile wanachokizalisha.

Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Katavi aliwaambia wakazi hao kwamba wafuate kanuni bora za kilimo na kuwasisitiza kulima mpunga kwa kufuata mistari ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa kila ekari.

Desemba 22, 2012 Waziri Mkuu atakuwa kata ya Kibaoni (kijijini kwao) ambapo atazungumza na wananchi kwenye uwanja wa shule ya msingi Kakuni.

Jiunge nasi kwenye social media
Facebook
Instagram
Youtube
Twitter

About The Author

Joachim Ernest Mushi, Kitaaluma ni mwanahabari muhitimu (Uandishi-2006) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC) kwa sasa Shule Kuu ya Uandishi na Mawasiliano. Nimekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi (Gazeti la Kulikoni & Thisday), Mwandishi mwandamizi Gazeti kongwe la Kiongozi, Mhariri wa Makala mwanzilishi wa Gazeti la Jambo Leo. Kwa sasa ni Mhariri Mkuu Kiongozi wa Thehabari.com, nchini Tanzania.

Related posts

Leave a Reply

Your email address will not be published.