watoto wapelekwe shule kukomesha ajira kwa watoto

mtoto akiwa kwenye ajira ya kubeba matofari ili kupata rizki
mtoto akiwa kwenye ajira ya kubeba matofari ili kupata rizki

Namwandishi wetu
Kilimanjaro.
VIONGOZI kuanzia ngazi za vitongoji hadi kata mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kuwafuatilia watoto ambao hawaendi shule na kuhakikisha wanasoma hatua ambayo itasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa watoto na watoto wa mitaani ambalo linazidi kukua kila kukicha.
Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na mwenyekiti wa wafanyabiashara wenye viwanda na Kilimo (TCCIA)Mkoani Kilimanjaro Bw. Patrick Boisafi, wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake kuhusiana na changamoto mbalimbali zinazolikabili kundi la watoto katika jamii ikiwemo tatizo la ajira kwa watoto pamoja na kuendelea kuwepo kwa vitendo vya kikatili dhidi yao.
Bw. Boisafi alisema tatizo la ajira kwa watoto katika jamii bado ni changamoto kubwa na kwamba inachangiwa na watoto kutokwenda shule hivyo ni vema viongozi wakahakikisha watoto wote walioko katika maeneo yao wanapata haki zao za kimsingi ikiwemo elimu hatua ambayo itawawezesha kuondokana na hali ya utegemezi hapo baadae na kukabiliana na changamoto za kimaisha.
Aidha alisema ni jukumu la viongozi kuhakikisha wazazi wanawapeleka watoto wao shule na kwa mzazi atakaye kikuka hilo achukuliwe sheria kali ikiwa ni njia moja wapo ya kudhibiti vitendo vya watoto kutopelekwa shule na kupunguza tatizo la ajira kwa watoto
“Sheria inasema ajira kwa watoto mwiko, lakini bado kuna ajira nyingi kwa watoto ikiwemo kazi za ndani umachinga na nyingine nyingi,kikubwa hapa ni kwamba watoto hawa walioko kwenye ajira hawakupata nafasi ya kwenda shule ndipo wakaamua kutafuta ajira ili kukabiliana na changamoto za kimaisha,na tatizo hili linaweza kukomeshwa endapo tu watoto wote watasomeshwa na kupata elimu na hili linapaswa kufuatiliwa na viongozi kuanzia ngazi za vitongoni hadi za juu, kwa kufanya hivyo tutaweza kupunguza kama si kumaliza vitendo vya ajira kwa watoto”alisema Bw. Boisafi.
Bw. Boisafi alisema kila mwaka juni 16 huadhimishwa siku ya mtoto Afrika na nchi yetu ni moja kati ya nchi ambazo huadhimisha siku hiyo, lakini pamoja na na maadhimisho hayo bado watoto wameendelea kunyanyasika katika jamii na kutendewa vitendo vya kikatili na vya kutisha huku matamko na mikakati ikiachwa kwenye makabrasha kusubiria mwaka mwingine.
Alisema ufike wakati sasa siku hiyo iadhimishwe kwa vitendo na kwa mwaka huu iwe ni siku ya kujipima na kufanya tathmini ya matukio ya kikatili kwa watoto kama yanapungua au yanaongezeka ili kuweza kuangalia ni nini cha kufanya kuondokana na vitendo hivyo badala ya kuendelea kufanya kwa mazoea huku watoto wakiendelea kutaabika na kuteseka katika jamii.
“Kila mwaka nimekuwa nikisikia maadhimisho ya watoto na katika siku hiyo ukihudhuria utasikia matamko mengi ambayo yanatolewa dhidi ya watoto lakini cha kushangaza mara baada ya kutoka kwenye maadhimisho hayo matamko na mikakati ambayo hupangwa huishia hapo na watoto hurudi manyumbani mwao na mitaani kuendelezewa vitendo vya kikatili,jambo hili si sahihi kabisa, ufike wakati sasa tubadilike na tuadhimishe siku hii kwa vitendo kukomesha vitendo vya kikatili kwa watoto kwani leo malalamiko mengi mitaani ni watoto kubakwa, kulawitiwa,kuteswa na hata kunyimwa haki zao za kimsingi ikiwemo elimu jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa nchi”alisema.
Katika hatua nyingine Bw. Boisafi aliwataka wazazi kusimama vema katika malezi na kuhakikisha watoto wanakua katika maadili yaliyomema ikiwa ni pamoja na kutimiziwa mahitaji yao ya kimsingi ikiwemo elimu.
Alisema ni vema pia wazazi wakaondokana na tabia ya kuwatwika watoto mizigo ya kulelea familia ili hali bado ni wadogo na hawana kazi halali zinazowaingizia fedha kutokana na kwamba, hali hiyo husababisha watoto wengi kujiingiza katika vitendo viovu na hatimaye kujikuta wanapata mimba na kupoteza ndoto za maisha yao.
“Katika jamii leo kuna mambo ya ajabu sana kwani wazazi wengi leo wamekuwa wakiwatumia watoto wao wa kike kupata fedha na wakati mwingine wamekuwa wakiwapangia majukumu ya kutekeleza manyumbani ili hali hakuna kazi anayofanya ya kumuingizia fedha na wakati mwingine utakuta ni mwanafunzi, jambo hili ni hatari sana na limechangia kwa kiasi kikubwa kuwaharibu watoto wetu wa kike, ni lazima likomeshwe kukuza kikazi chenye maadili”alisema

Jiunge nasi kwenye social media
Facebook
Instagram
Youtube
Twitter

About The Author

Joachim Ernest Mushi, Kitaaluma ni mwanahabari muhitimu (Uandishi-2006) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC) kwa sasa Shule Kuu ya Uandishi na Mawasiliano. Nimekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi (Gazeti la Kulikoni & Thisday), Mwandishi mwandamizi Gazeti kongwe la Kiongozi, Mhariri wa Makala mwanzilishi wa Gazeti la Jambo Leo. Kwa sasa ni Mhariri Mkuu Kiongozi wa Thehabari.com, nchini Tanzania.

Related posts

Leave a Reply

Your email address will not be published.