Walimu mkoani Mara waahidi kuendeleza mgomo hadi kieleweke

Rais wa CWT, Gratian Mukoba
Rais wa CWT, Gratian Mukoba

*Tarime wanafunzi waandamana kudai masomo

Na Shomari Binda, Musoma

CHAMA cha walimu Mkoa wa Mara (CWT) kimesema kitaendelea na mgomo ulioanza jana bila kikomo mpaka pale viongozi wao wa Kitaifa watakapo wapa taarifa juu ya kutekelezewa madai yao mbalimbali ambayo wamekuwa wakiyadai kwa muda mrefu na kushindwa kutimiziwa.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa Chama cha walimu Mkoa wa Mara Fatuma Bakari alipokuwa akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake juu ya hatima ya mgomo huo ambao gazeti hili lilifika katika baadhi ya shule Mjini Musoma na kukuta matangazo yaliyowazuia walimu kuingia madarasani.

Alisema haiwezekani walimu kuendelea kunyanyaswa ki maslahi na kuonekana kazi wanayoifanya si lolote katika jamii na kupelekea kuendelea kuishi maisha ya dhiki na duni huku Serikali ikiendelea kulikalia kimya suala hilo.

Katibu huyo wa CWT Mkoa wa Mara alidai kuwa haiwezekani katika waraka Na.1/2012 wa mishahara wa Serikali mwalimu akiongezewa kiasi cha shilingi 33,000 kutoka mshahara wa laki mbili na arobaini na nne elfu (244,000) hadi laki mbili na sabini na saba elfu (277,000) huku afisa elimu akiongezea zaidi ya shilingi laki mbili kutoka laki mbili hamsini na sita elfu (256,000) hadi laki nne na elfu mbili.

“Suala hili ndugu mwandishi haliwezekani na pale tunapofanya mgomo huu Watanzania inabidi watuelewe na wasituone watu tusiofaa katika jamii maana madai tunayoyadai ni ya muda mrefu na hatuwezi kuendelea kuwa katika hali hii,” alisema Fatuma.

KATIKA hali isiyo ya kawaida Wanafunzi wa Shule mbalimbali za Msingi Wilayani Tarime wameandamana hadi ofisi ya Ofisa Elimu Wilaya ya Tarime mkoani mara wakidai haki zao za kupata elimu baada ya walimu wao kugoma kuingia madarasani na kisha kuwataka wanafunzi kuondoka kwenda majumbani kwao.

Wanafunzi hao walisikika wakiimba na kuongea mbele ya Ofisa elimu wa Wilaya Emanuel Jonson katika viwanja vya ofisi ya elimu Wilaya, wakisema kitendo cha walimu kugoma kufundisha kinawathiri wanafunzi hasa wanaoenda kumaliza elimu ya msingi hivi karibuni.

“Watoto tunataka haki zetu, Watoto tunataka kupata elimu, watoto tunataka kusoma tunaomba walimu walipwe madai yao tuingie madarasani, watoto tusinyimwe haki yetu ya kupata elimu walimu wanapogoma waathirika ni sisi wanafunzi Serikali tatueni mgomo wa walimu,” walisema wanafunzi hao.

Ofisa elimu Johnsoni aliwatuliza watoto hao na kuhaidi kutatua tatizo la walimu wao ambapo aliwataka wanafunzi wote kurejea shuleni kuendelea na masomo yao.

Jonsoni alisema kuwa anasikitika kwa kitendo cha walimu kutoingia madarasani na kwamba kitendo hicho ni kupunguza stahili za watoto ambapo amewataka walimu wote kuhudhulia madarasani na kwamba ambao hawatohudhuria vipindi watawahibishwa .

“Kwa maelezo ya Serikali mgomo ni batiri nimefanya kikao na waratibu elimu wote kuwaelekeza kwenda katani kwao kuwahimiza walimu kurejea shuleni na kwa mujibu wa maelekezo Serikali tumetoa taratibu za kujaza fomu kwa walimu wote za kuthibitisha anaeunga mgomo au asiyeunga mgomo kwa wale ambao watagoma watachukuliwa hatua.” alisema Jonson

Kuandamana kwa wanafunzi hao ni baada ya walimu kutoka katika shule mbalimbali za msingi Wilayani Tarime kugoma baada ya Serikali kushindwa kutekeleza mahitaji yao ya posho za kufundishia, Nyongeza ya mshahara na posho za mazingira hatarishi ya kazi.

Mwenyekiti wa chama Cha Walimu Wilayani Tarime Matinde Magabe alisema kuwa mgomo huo ni endelevu hadi pale Mwenyekiti wa CWT Taifa atakapotoa tamko na kwamba hata kesho hawatoingia darasani.

“Mgomo ni halali tunataka Serikali itulipe nyongeza ya mshahara kwa asilimia 100%, posho ya kufundishia asilimia 55 kwa walimu wa sayansi na hesabu asilimia 50 ya mshahara kwa walimu wa masomo ya sanaa, posho ya mazingira magumu ya kazi asilimia 30% na mgomo huu ni endelevu,” alisema Magabe. Magabe alisema kuwa Wilaya ya Tarime inajumla ya walimu wapatao 2870 kati yao ni wa shule za msingi, Sekondari na walimu wa chuo cha walimu Tarime.

Jiunge nasi kwenye social media
Facebook
Instagram
Youtube
Twitter

About The Author

Joachim Ernest Mushi, Kitaaluma ni mwanahabari muhitimu (Uandishi-2006) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC) kwa sasa Shule Kuu ya Uandishi na Mawasiliano. Nimekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi (Gazeti la Kulikoni & Thisday), Mwandishi mwandamizi Gazeti kongwe la Kiongozi, Mhariri wa Makala mwanzilishi wa Gazeti la Jambo Leo. Kwa sasa ni Mhariri Mkuu Kiongozi wa Thehabari.com, nchini Tanzania.

Related posts

Leave a Reply

Your email address will not be published.