Vitambulisho vya raia EAC kutumika kama paspoti za kusafiria

Mchakato wa vitambulisho vya taifa Tanzania
Mchakato wa vitambulisho vya taifa Tanzania

Na Mwandishi wa EANA, Arusha

KUNA uwezekano kwamba vitambulisho vya kitaifa walivyonavyo raia wa Afrika Mashariki vinaweza siku moja kutumika kama hati mbadala ya kusafiria ndani ya kanda hiyo, iwapo hatua iliyoanzishwa na Kenya na Rwanda itaenezwa katika nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Nchi nyingine wanachama wa EAC ni pamoja na Tanzania, Uganda na Burundi.

“Kenya tayari ina mipango ambayo iko mbioni kuingia katika makubaliano na Rwanda kuruhusu raia wa nchi mbili hizo kuwa huru kuvuka mipaka kati yao kwa kutumia vitabulisho vya utaifa wao,” alisema Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki, Musa Sirma.

Sirma, ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano Afrika Mashariki wa Kenya aliongeza kuwa nchi hizo mbili pia zitabadilishana maafisa wa uhamiaji kutoa huduma kwenye kaunta za mataifa yao.

“Huo ndio mwanzo wa kuyafanya mataifa yote matano ya EAC kuondoa mahitaji ya hati za kusafiria miongoni mwa raia wake kama walivyoweza kuondoa viza kwa wasafiri wa ndani ya kanda ,” Sirma alibainisha.

Waziri aliyasema hayo mjini Kigali, Rwanda katika mkutano wa Tano wa Vyombo vya Habari vya Afrika Mashariki uliandaliwa na Sekretarieti ya EAC kwa kushirikiana na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki kwa kuungwa mkono na Trade-Mark East Africa.

Kenya na Rwanda tayari zimeshatoa vitambulisho vyake vya taifa ambapo Tanzania inaendelea na mchakato wa kufanya hivyo huku hakuna harakati zozote za aina hiyo kwa nchi za Uganda na Burundi.

Robert Mugabe, ambaye ni Mhariri Mkuu wa Chapisho la ‘Great Lakes’ Voice,’ ambaye hana uhusiano na Rais wa Zimbabwe, alisema hati za kusafiria ni ghali kwa raia wa Afrika Mashariki kwa sababu nchini Rwanda inawagharimu sawa na dola za Kimarekani 100 (zaidi ya shilingi 150,000/-).

“Ninafurahi sana kusikia kuwa hivi karibuni itakuwa bure kwenda Kenya kuliko ilivyokuwa huko nyuma nilipompeleka mama yangu kwa matibabu na kulazimika kulipia hati yake ya kusafiria kwa dola za Kimarekani mbali na gharama za matibabu,” Mugabe alisema na kuongeza kuwa ilikuwa ni vigumu hata kwa waandishi wa habari waliohitaji kuvuka mipaka mara kwa mara.

EAC imekuwa ikitoa hati za kusafiria za jumuiya hiyo ambayo mbali na kutumika kwa kusafiria kwa wanachama wa mataifa hayo iliwahakikishia wamiliki wake kipindi cha kubaki nchi wanayotembelea kwa miezi sita lakini kuondolewa hivi karibuni kwa viza miongoni mwa nchi wanachama wa EAC imepelekea kutokutumika kwake kwa sasa.

Mwandishi Mkongwe Jenerali Ulimwengu kutoka Tanzania hapo awali aliipongeza serikali ya Rwanda kwa kufungua milango kwa raia kutoka mataifa mengine manne ya EAC wanaotaka kufanya kazi au kuishi nchini humo kama wangependa kufanya hivyo.

Wakati huohuo, ilibainika pia katika mkutano huo kuwa ufufuaji wa reli ya Afrika Mashariki ni ufumbuzi pekee wa kupambana na vikwazo vinavyoathiri mwingiliano wa kibiashara ndani ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Jiunge nasi kwenye social media
Facebook
Instagram
Youtube
Twitter

About The Author

Joachim Ernest Mushi, Kitaaluma ni mwanahabari muhitimu (Uandishi-2006) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC) kwa sasa Shule Kuu ya Uandishi na Mawasiliano. Nimekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi (Gazeti la Kulikoni & Thisday), Mwandishi mwandamizi Gazeti kongwe la Kiongozi, Mhariri wa Makala mwanzilishi wa Gazeti la Jambo Leo. Kwa sasa ni Mhariri Mkuu Kiongozi wa Thehabari.com, nchini Tanzania.

Related posts

Leave a Reply

Your email address will not be published.