Mnyika ahojiwa na Polisi Singida, atoa maelezo ya kurasa 12

Mbunge wa Jimbo la Ubungo (CHADEMA), John John Mnyika.
Mbunge wa Jimbo la Ubungo (CHADEMA), John John Mnyika.

Na Mwandishi Wetu, Singida

MBUNGE wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika amehojiwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida ikiwa ni kuhusiana na mkutano uliofanywa na chama hicho ambao ulihusishwa na vurugu zilizosababisha kuuwawa kijana mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mnyika alienda mkoani Singida baada ya wito wa Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa huo kwa mahojiano maalumu. Akizungumza mara baada ya mahojiano alisema; “Nimemaliza kutoa maelezo ya kurasa 12 pamoja na mambo mengine nimesema wazi kuwa kabla ya mkutano nilipewa taarifa kuwa kuna kikundi cha vijana wa CCM kimepangwa kuvuruga mkutano, hata baada ya kuwaambia Polisi wahakikishe ulinzi, Polisi waliwaachia vijana hao warushe mawe wakati Bwana Waitara akihutubia.”

Aidha Mnyika alilieleza Jeshi la Polisi mkoani humo kuwa taarifa za mauaji walizipata usiku baada ya kurejea Singida Mjini na zilitolewa na RPC mwenyewe.

“Hivyo sifahamu uhusiano wowote uliopo kati ya mauaji na mkutano wa CHADEMA uliomalizika kwa amani. Na nimewaambia sikutoa lugha yoyote ya matusi wala uchochezi bali nilieneza sera na wananchi wakataka turudi tena na tukawaahidi kuwa tulikwenda kwenye maandalizi ya Operesheni Sangara ya Singida nzima,” alisema.

“Nimewaambia, tuna ushahidi wa video na tutautoa mahakamani,” alisema mbunge huyo. Mnyika alifika mkoani Singida mapema kufuatia mwito wa Polisi kutoa maelezo kuhusu mkutano alioufanya Iramba, lakini mahojiano yalishindwa kufanyika muda huo kwa madai walikuwa wakisubiriwa kikosi cha upelelezi toka Dar es Salaam.

Jiunge nasi kwenye social media
Facebook
Instagram
Youtube
Twitter

About The Author

Joachim Ernest Mushi, Kitaaluma ni mwanahabari muhitimu (Uandishi-2006) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC) kwa sasa Shule Kuu ya Uandishi na Mawasiliano. Nimekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi (Gazeti la Kulikoni & Thisday), Mwandishi mwandamizi Gazeti kongwe la Kiongozi, Mhariri wa Makala mwanzilishi wa Gazeti la Jambo Leo. Kwa sasa ni Mhariri Mkuu Kiongozi wa Thehabari.com, nchini Tanzania.

Related posts

Leave a Reply

Your email address will not be published.