Madaktari tatizo Hospitali ya Mawenzi Kilimanjaro

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama (wa kwanza kulia) akitoa hotuba yake katika uzinduzi huo huku mgeni rasmiMama Tunu Pinda  akifuatilia kwa makini.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama (wa kwanza kulia) akitoa hotuba yake katika uzinduzi huo huku mgeni rasmiMama Tunu Pinda akifuatilia kwa makini.

Na Mwandishi Wetu, Moshi

HOSPITALI ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa madaktari hali ambayo inasababisha huduma zinazotolewa kutokukidhi haja za walengwa.

Hayo yamebainishwa na mganga mkuu wa mkoa huo Dk. Mtumwa Mwako wakati wa uzinduzi wa mradi wa matanki ya maji yenye ujazo wa lita 40,000 uliofadhiliwa na kampuni ya bia ya Serengeti Breweries Limited ambao umegharimu zaidi ya Sh. mil. 60 .

Dk. Mwako alisema hospitali hiyo ambayo ilianza mwaka 1920 kama zahanati na kupandishwa daraja mwaka 1956 na kuwa hospitali ya mkoa wa Kilimanjaro, inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi kwa asilimia 72 ya mahitaji hususani madaktari bingwa, hali ambayo inakwamisha juhudi za serikali za utoaji huduma bora kwa wagonjwa.

Alisema hospitali hiyo ambayo hupokea wagonjwa 500 hadi 1,000 kwa siku inawatumishi 488 kati yao madaktari bingwa ni watano pekee, madaktari wa kawaida ni Nane, daktari wa meno mmoja, wafamasia watatu, madaktari wasaidizi 23, matabibu 17, wauguzi 95, wauguzi wakunga 62 pamoja na fundi sanifu maabara sita.

Dk. Mwako alisema changamoto nyingine inayoikabili hospitali hiyo ni ukosefu wa chumba cha upasuaji ambacho kilifungwa mwaka 2010 kwa kutokidhi viwango hali ambayo inasababisha wananchi kukosa huduma za upasuaji mdogo na mkubwa.

Alisema changamoto nyingine ni Uchakavu wa majengo ya hospitali pamoja na msongamano wa wagonjwa katika idara na wodo kadha hali ambayo inasababisha wahudumu kuelemewa.

Dk. Mwako akizungumzia tatizo la maji katika hospitali hiyo alisema kutokana na hali ya ukame uliochangiwa na uharibifu wa mazingira maji yamekuwa ni tatizo kubwa na kwamba mahitaji yanayohitajika hospitalini hapo ni lita za ujazo 200,000 kwa siku na kwa mwaka ni lita 72,000,000.

Akizindua mradi huo mke wa waziri Mkuu Bi. Tunu Pinda aliipongeza kampuni ya SBL kwa ufadhili wao katika sekta za kijamii na kutoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kutoa msaada wa matanki ya uhifadhi maji katika hospitali hiyo ambapo kwa sasa inahitaji matanki ya kuhifadhi kiasi cha lita za ujazo 160,000 ili kutatua tatizo zima la maji hospitalini hapo.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama alisema serikali ya mkoa huo itashirikiana kwa karibu na uongozi wa hospitali ili kuhakikisha huduma zitolewazo zinaendelea kuboreshwa.

Jiunge nasi kwenye social media
Facebook
Instagram
Youtube
Twitter

About The Author

Joachim Ernest Mushi, Kitaaluma ni mwanahabari muhitimu (Uandishi-2006) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC) kwa sasa Shule Kuu ya Uandishi na Mawasiliano. Nimekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi (Gazeti la Kulikoni & Thisday), Mwandishi mwandamizi Gazeti kongwe la Kiongozi, Mhariri wa Makala mwanzilishi wa Gazeti la Jambo Leo. Kwa sasa ni Mhariri Mkuu Kiongozi wa Thehabari.com, nchini Tanzania.

Related posts

Leave a Reply

Your email address will not be published.