Leodiger Tenga aongoza maelfu kumzika mwenyekiti wa chama cha Soka Mara

baadhi ya waombilezaji katika msiba huo
baadhi ya waombilezaji katika msiba huo

Na mwandishi wetu

Musoma

RAIS wa shirikisho la soka hapa Nchini (TFF) Leodiger Tenga ameongoza maelfu ya waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha soka Mkoani Mara (FAM) na mjumbe wa kamati ndogo ya mahesabu ya (TFF) Fabian Samo yaliyofanyika nyumbani kwake maeneo ya Nyakato katika Manispaa ya Musoma.

Akisoma salamu za rambirambi kutoka Shirikisho la soka hapa Nchini,Tenga alisema wamepata pengo kubwa kwa kuondokewea na kiongozi huyo kwa kile alichokieleza bado mchango na mawazo ya kiongozi huyo yalikuwa yakihitajika kutokana na uwezo wake mkubwa aliokuwa nao katika masuala ya mahesabu.

Alisema Samo alikuwa mwepesi wa kuhudhulia vikao pale alipokuwa akihitajika na alichangia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha uwezo wake aliokuwa nao katika masuala ya mahesabu anayatoa katika shirikisho hilo na imepelekea kuwa na uangalizi mzuri katika kusimamia masuala ya fedha.

Tenga ameeleza kuwa uwezo mkubwa aliokuwa nao Fabian Samo ndio uliopelekea wadau wa soka katika Mkoa wa Mara kumchagua kwa vipindi viwili kukiongoza chama cha mpira wa miguu (FAM) na katika kipindi hicho kumekuwa na mabadiliko makubwa katika soka la Mkoa wa Mara.

Rais huyo wa TFF amewaomba wadau wa soka Mkoani Mara kufata yale yote mazuri aliyoyafanya marehemu Fabian Samo ili kupitia hayo soka la Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla liweze kundelea na kupanda na kuwaomba viongozi wengine katika Soka la Mkoa wa Mara kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba na kudai kuwa TFF ipo pamoja katika kipindi hiki cha msiba.

Akitoa salamu kwa upande wa Serikali kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara John Tuppa ambaye pia alikuwepo msibani hapo Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara Makongoro Nyerere alisema licha ya kujishughulisha na kupenda masuala ya michezo marehemu Fabian Samo alikuwa ni kiongozi mzuri katika masuala ya siasa na kiongozi mvumilivu tangu alipokuwa Diwani na makamo Mwenyekiti wa Halimashauri ya Wilaya ya Musoma kwa kipindi cha miaka 10.

Makongoro alisema ili kumuenzi kiukweli marehemu Fabian Samo ni kufuata yale yote mazuri aliyoyaacha kwa dhati na kuwa wawazi katika masuala ya uongozi kama ambavyo alikuwa akifanya kiongozi huyo.

Akizungumza kwa niaba ya wadau wa soka katika kutoa saramu za rambirambi,aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha soka zamani (FAT) Michael Wambura alisema pengo walilopata wadau wa soka kufuatia kifo cha Fabian Samo halitazibika kutokana na moyo aliokuwa nao katika kusimamia masuala ya mpira.

Wambura alisema ni wajibu wa kila mdau kuiga mazuri yote yaliyofanywa na Fabian Samo katika kusimamia haki na kuwa wawazi katika kusimamia ukweli ili kuweza kuendeleza soka la Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla.

Viongozi wengine waliohudhulia mazishi hayo ni Waziri wa kazi na na ajira Gaudensia Kabaka,Mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini Nimrod Mkono,M kuu wa wilaya ya Bunda Joshua Mirumbe na mstahiki Meya wa Manispaa ya Musoma Alex Kisulula.

marehemu Fabian Samo alizaliwa mwaka 1944 katika kijiji cha Wegero Wilaya ya Musoma vijijini ameacha mjane,watoto 12 na wajukuu 17.

Mungu ailaze roho ya Marehemu Fabian Samo mahali pema peponi

Jiunge nasi kwenye social media
Facebook
Instagram
Youtube
Twitter

About The Author

Joachim Ernest Mushi, Kitaaluma ni mwanahabari muhitimu (Uandishi-2006) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC) kwa sasa Shule Kuu ya Uandishi na Mawasiliano. Nimekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi (Gazeti la Kulikoni & Thisday), Mwandishi mwandamizi Gazeti kongwe la Kiongozi, Mhariri wa Makala mwanzilishi wa Gazeti la Jambo Leo. Kwa sasa ni Mhariri Mkuu Kiongozi wa Thehabari.com, nchini Tanzania.

Related posts

Leave a Reply

Your email address will not be published.