JK aenda Uganda kuhudhuria ICGLR

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisindikizwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam  Mhe Saidi Mecky Sadik  kabla ya kuanza safari ya kwenda Kampala, Uganda,kuhudhuria mkutano wa nchi za Maziwa Makuu asubuhi Agosti 8, 2012
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisindikizwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Saidi Mecky Sadik kabla ya kuanza safari ya kwenda Kampala, Uganda,kuhudhuria mkutano wa nchi za Maziwa Makuu asubuhi Agosti 8, 2012

Na Mwandishi Maalumu

RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete atakuwa miongoni mwa wakuu wa nchi na Serikali watakaoshiriki katika mkutano maalum wa nchi wanachama wa Taasisi ya Kimataifa ya Nchi za Maziwa Makuu – International Conference on the Great Lakes Region (ICGLR) unaoanza mjini Kampala, Uganda, baadaye, Agosti 7, 2012.
Mkutano huo wa siku mbili utajadili hali tete ya usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako mapigano kati ya Jeshi la DRC na kikundi cha waasi cha M23 yamesababisha zahama ya vifo na maelfu ya wakimbizi kutoka Jimbo la Kivu Kaskazini.
Inakadiriwa kuwa kiasi cha wakimbizi 30,000 wamevuka mipaka na kuingia katika Burundi na Rwanda kukimbia mapigano hayo yaliyoanza upya Aprili, mwaka huu.
Rais Kikwete na ujumbe wake wameondoka nchini asubuhi ya leo kwenda Uganda kwa ajili ya mkutano huo wa siku mbili na ambao umetanguliwa na mikutano ya Waratibu wa Kitaifa wa nchi wanachama wa ICGLR na ule wa mawaziri wa ulinzi na mambo ya nchi hizo.
Mkutano huo unaofanyika chini ya uenyekiti wa Mwenyekiti wa sasa wa ICGLR, Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda ni matokeo ya uamuzi wa mkutano mwingine maalum wa ICGLR uliofanyika wakati wa Mkutano wa 19 wa kawaida wa Umoja wa Afrika (AU) Julai 15, mwaka huu, mjini Addis Ababa, Ethiopia. Ilikubaliwa katika mkutano huo maalum kuitisha mkutano mwingine maalum kujadili hali hiyo.
Aidha, mkutano huo wa Addis Ababa ulielezea masikitiko yake kuhusu hali tete ya usalama Mashariki mwa DRC na kulaani vikali kuibuka na vitendo vya kikundi cha M23. Mkutano huo ulisisitiza kuwa jumuia ya kimataifa ihakikishe haitoi msaada wa aina yoyote kwa kikundi hicho ama vikundi vingine hasi vinavyoyumbisha Mashariki mwa DRC.
Mkutano huo wa Addis Ababa pia uliunga mkono jitihada zinazoendelezwa na Serikali ya DRC kupambana na M23 na pia uliunga mkono jitihada za pamoja za DRC na Rwanda kujaribu kurekebisha hali ya usalama katika eneo la Mashariki mwa Congo.
Kikundi cha M23 kinaundwa na wapiganaji ambao walijitenga kutoka Jeshi la DRC mapema mwaka huu. Kikundi hicho kinapata jina lake kutoka tarehe ya Machi 23, mwaka 2009, wakati makubaliano yalipofikiwa kati ya Serikali ya DRC na kikundi cha waasi cha zamani cha Congres National pour la Defense du Paople (CNDP) ambacho baadaye kilikiuka makubaliano hayo kwa kukataa kujiunga katika Jeshi la Ulinzi la Congo (FARDC).

Jiunge nasi kwenye social media
Facebook
Instagram
Youtube
Twitter

About The Author

Joachim Ernest Mushi, Kitaaluma ni mwanahabari muhitimu (Uandishi-2006) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC) kwa sasa Shule Kuu ya Uandishi na Mawasiliano. Nimekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi (Gazeti la Kulikoni & Thisday), Mwandishi mwandamizi Gazeti kongwe la Kiongozi, Mhariri wa Makala mwanzilishi wa Gazeti la Jambo Leo. Kwa sasa ni Mhariri Mkuu Kiongozi wa Thehabari.com, nchini Tanzania.

Related posts

Leave a Reply

Your email address will not be published.