ECOWAS Kuongeza Vikosi Vyake Mali

Baadhi ya viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi
Baadhi ya viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi

MATAIFA ya Afrika Magharibi yamekubali kuongeza idadi ya wanajeshi wake watakaopelekwa Mali kuwaunga mkono wanajeshi wa nchi hiyo kupambana na waasi wenye itikadi kali za Kiislamu. Uamuzi huo umefikiwa wakati ambapo vikosi vya Mali na Ufaransa vikidhibiti maeneo muhimu ya Gao. Viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi-ECOWAS waliokutana mjini Abidjan, Cote d’Ivoire wamefikia uamuzi huo ambapo sasa wanajeshi watakaopelekwa Mali watakuwa 7,700 badala ya 3,300 waliokubaliana awali.

Mkuu wa Majeshi wa Cote d’Ivoire, Jenerali Soumaila Bakayoko amesema kuwa hadi sasa wanajeshi 1,750 kutoka nchi jirani za Afrika Magharibi wako Mali, huku Chad na Niger zikitoa wanajeshi 550 kila mmoja.

Nchini Mali kwenyewe, vikosi vya Mali na Ufaransa vimefanikiwa kuudhibiti uwanja wa ndege na daraja muhimu katika mji wa Gao. Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian amesema kuwa wanajeshi hao wameudhibiti mji huo uliokuwa ukidhibitiwa na waasi tangu mwezi Juni mwaka uliopita na kwamba ngome kuu na magari ya waasi yameharibiwa.

Msemaji wa jeshi la Ufaransa, Emmanuel Dosseur, amesema katika operesheni za kijeshi zinazoendelea eneo la Magharibi, wanajeshi walikuwa katika mji wa Lere uliopo umbali wa kilometa 440 kutoka Timbuktu. Watu walioshuhudia wamesema kuwa jeshi kubwa limeonekana katika mji wa Sevare uliopo umbali wa kilometa 570 kusini mwa mji wa Gao.

Wakati huo huo, Rais Barack Obama wa Marekani amekubali ombi la Rais Francois Hollande wa Ufaransa la kujaza mafuta ndege za kivita za Ufaransa ambazo zinaendesha operesheni dhidi ya waasi wa Mali. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, George Little amesema viongozi hao pia wamejadiliana kuhusu mipango ya Marekani kusafirisha wanajeshi kutoka mataifa ya Afrika katika jitihada za kuunga mkono juhudi za kimataifa katika suala la Mali.

Aidha, Umoja wa Ulaya umesema jana kuwa utaanza kupeleka wakufunzi wa kijeshi ili kuwapatia mafunzo wanajeshi wa Mali katikati ya mwezi Februari huku wakufunzi wote 200 hadi 250 wakiwa Mali ifikapo katikati ya mwezi Machi. Ujerumani imegusia uwezekano wa kuiunga mkono Mali katika mkutano ujao wa wafadhili. Viongozi wa Umoja wa Afrika wanakutana leo mjini Addis Ababa, Ethiopia, ambapo pamoja na mambo mengine wataujadili mzozo wa Mali, likiwemo suala la kupelekwa haraka kwa kikosi cha Afrika nchini humo.

Kamishna wa Amani na Usalama wa umoja huo, Ramtane Lamamra, amesema kuwa nchi wanachama watapewa muda wa wiki moja kuandaa wanajeshi watakaopelekwa katika operesheni ya kijeshi nchini Mali chini ya vikosi vya kimataifa vitakavyoongozwa na Umoja wa Afrika-AFISMA. Umoja huo pia utaomba msaada wa muda wa kimkakati kutoka kwenye Umoja wa Mataifa kwa ajili ya AFISMA na kuuomba umoja huo kuidhinisha kuanzishwa haraka mipango ambayo itaiwezesha AFISMA kupeleka haraka wanajeshi wake na kupewa mamlaka ya kuendesha operesheni. Msaada wa kimkakati utajumuisha usafiri, madawa na hospitali katika maeneo ya mapambano.
-DW

Jiunge nasi kwenye social media
Facebook
Instagram
Youtube
Twitter

About The Author

Joachim Ernest Mushi, Kitaaluma ni mwanahabari muhitimu (Uandishi-2006) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC) kwa sasa Shule Kuu ya Uandishi na Mawasiliano. Nimekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi (Gazeti la Kulikoni & Thisday), Mwandishi mwandamizi Gazeti kongwe la Kiongozi, Mhariri wa Makala mwanzilishi wa Gazeti la Jambo Leo. Kwa sasa ni Mhariri Mkuu Kiongozi wa Thehabari.com, nchini Tanzania.

Related posts

2 Comments

  1. omar

    Kidonda imepona Waafrica wamesahau ukoloni wazungu ubeberu na utumwa waliokuwa wanafanyiwa na hawahawa wanaowaita mabwana zetu kutatua matatizo yao na ni hawa mabwana wazungu wanaokoroga dunia kwa kuangusha mabomu hatari kuanzia vietnam, kambodia, pakistan,afghanistan,irak, libya ,syria, na sasa mali,swali hii au lego lao ni nini?jibu ni mali yenu ya asili kama madini na mafuta na ardhi kama wanavyomuadhibu Mugabe kwa ajili ya ardhi yake na madini na vilevile akili yenu haichaji kwa nini walimuua Gadafi wakati hakuwa tishio lolote kwao isipokua lengo lao ni nini? mafuta basi.

    Reply
  2. omar

    Waafrica kuna kitu inaitwa Africom maana yake nini ?maana yake ni sisi hatujiamini kulinda mipaka yetu na hatujiamini kwa hiyo mje kutulinda nyie wazungu mabwana wetu mliotutawala zamani na bado tunawahitaji.

    Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published.