Clinton azipongeza serikali za Sudan kumaliza mzozo

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Hillary Rodham Clinton (kushoto) akiwa na mmoja wa viongozi wa juu wa Sudan.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Hillary Rodham Clinton (kushoto) akiwa na mmoja wa viongozi wa juu wa Sudan.

VIONGOZI nchini Marekani na Ulaya wamesifu makubaliano yaliyofikiwa Agasti 04, 2012 kati ya Sudan na Sudan Kusini kumaliza mzozo wa mafuta, ambao umesababisha matokeo mabaya ya kiuchumi na kutishia vita.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Hillary Rodham Clinton , ambaye amefanya ziara Sudan ya Kusini kama sehemu ya ziara yake katika bara la Afrika, alitoa sifa hizo kwa nchi zote mbili.

“Tunapongeza ujasiri wa uongozi wa jamhuri ya Sudan ya kusini kwa kuchukua uamuzi huu”, alisema na kuendelea; “Muda sasa umefika kumaliza mzozo wa mafuta, kwa ajili ya hali bora ya maisha ya watu wa Sudan ya Kusini na matarajio yao ya hali bora ya baadaye kutokana na changamoto zinazotokea”.

Amedokeza kuwa makubaliano hayo yanaipa Sudan, nafasi ya kujitoa katika mfadhaiko mkubwa wa kiuchumi ambao unaikumba nchi hiyo. Iwapo Sudan nayo pia itachukua hatua kuelekea amani katika majimbo ya Kordofan ya kusini, Blue Nile na Darfur, na iwapo itaheshimu haki za binadamu za raia zake wote, pia nayo inaweza kuwapa watu wake maisha bora ya baadaye, Clinton alisema.

Rais wa Marekani Barack Obama pia amesifu makubaliano hayo. Marekani itaendelea kuunga mkono juhudi za kuendeleza amani ya kudumu kwa watu wa Sudan na Sudan ya kusini, Obama amesema katika taarifa. Nazihimiza pande hizo mbili kutumia kasi iliyopo kutokana na mafanikio haya kutatua masuala yaliyobakia ya mipaka na usalama.

Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa umoja wa Ulaya, anayehusika na masuala ya mambo ya kigeni, Catherine Ashton, amesema kuwa anakaribisha taarifa hizo.

“Nazipongeza serikali zote mbili kwa kufikia muafaka ambao umewezesha makubaliano haya na natumai kuwa hali hiyo sasa itaonyeshwa pia katika masuala mengine yaliyobaki, ikiwa ni pamoja na mipaka, jimbo la Abyei na mipango ya usalama,” Ashton aliongeza.

Mafanikio hayo yalitangazwa mapema Jumamosi, wakati mpatanishi mkuu Thabo Mbeki alipowaambia waandishi habari kuwa “mafuta sasa yataanza kutiririka tena”, katika taarifa aliyoitoa katika mkutano wa baraza la usalama na amani la umoja wa Afrika, katika mji mkuu wa Ethiopia , Addis Ababa.

Baraza hilo lilikutana kujadili jinsi ya kutatua mzozo huo kati ya nchi hizo mbili baada ya kushindwa kufikia makubaliano juu ya usalama na mafuta, kabla ya kumalizika muda wa mwisho uliowekwa na baraza la usalama la umoja wa mataifa wa Agasti 2.

Januari, Sudan ya Kusini ilifunga uzalishaji wa mafuta baada ya Sudan kutaifisha mafuta ghafi yenye thamani ya dola milioni 815 ya Sudan kusini, ambayo imedai ni malipo ya ushuru ambao haujalipwa.

Mei mwaka huu, umoja wa mataifa uliamuru kwa kitisho cha kuweka vikwazo kuwa pande hizo mbili zisitishe uhasama, ziondoe majeshi yao kutoka katika jimbo linalogombaniwa la Abyei na kukubaliana malipo ya ushuru wa mafuta katika muda wa miezi mitatu.

Mazungumzo mengine yamesitishwa hadi baada ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan baadaye mwezi huu.

-DW

Jiunge nasi kwenye social media
Facebook
Instagram
Youtube
Twitter

About The Author

Joachim Ernest Mushi, Kitaaluma ni mwanahabari muhitimu (Uandishi-2006) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC) kwa sasa Shule Kuu ya Uandishi na Mawasiliano. Nimekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi (Gazeti la Kulikoni & Thisday), Mwandishi mwandamizi Gazeti kongwe la Kiongozi, Mhariri wa Makala mwanzilishi wa Gazeti la Jambo Leo. Kwa sasa ni Mhariri Mkuu Kiongozi wa Thehabari.com, nchini Tanzania.

Related posts

Leave a Reply

Your email address will not be published.