SARA DUMBA ASIFU JUKWAA LA ALIZETI


SARA DUMBA

Na William Macha-Iringa

MKUU wa Wilaya ya Njombe, Sara Dumba amelimwagia sifa Jukwaa la Alizeti lililozinduliwa mkoani Iringa, kupitia mradi wa Muunganisho Ujasiriamali Vijijini (MUVI) lilowakutanisha wadau anuai wa masuala ya kilimo na tafiti.
Akizungumzia jukwaa hilo, Dumba amesema wakulima wa alizeti mkoani Iringa kwa kipindi kirefu wamekuwa wakizalisha mazao kwa uzoefu, lakini sasa wanapaswa kutumia nyenzo za kisasa na kufuata ushauri kutoka MUVI.
“Jukwaa hili ni muhimu kwa wakulima wa alizeti kwani ni chombo kinachotoa mwongozo na kuwajengea uwezo wazalishaji ili waweze kuzalisha kwa wingi na kuwa na uhakika wa soko,” alisema Dumba.
Aliongeza kuwa wakulima wanapaswa kufahamu kuwa alizeti ni zao linaloweza kuwainua kiuchumi kama watafuata kanuni zote za uzalishaji ikiwa ni pamoja na matumizi mazuri ya mbegu aina ya RECOD waliyoshauriwa na wataalam kutoka MUVI.
Katika hatua nyingine amevisisitiza vikundi mbalimbali vya uzalishaji ambavyo tayari vimeundwa katika mkoani Njombe na Iringa kuhakikisha kwamba vinakuwa na kauli moja ili kuweza kufikia mafanikio katika uzalishaji wa zao hilo.
Akizindua jukwaa hilo Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa , Dk. Christine Ishengoma, ameupongeza Mradi wa Muungano Ujasiriamali Vijijini (MUVI) kwa kuweza kuwaunganisha wajasiriamali katika ngazi mbalimbali za wilaya, mkoa na hatimaye taifa.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo,mkuu wa wilaya ya Iringa, Asseri Msangi amesema kuwa lengo kuu la mradi wa MUVI ni kukuza na kuimarisha biashara za wajasiriamali hasa wale wa vijijini ambao kwa sehemu kubwa shughuli zao zinategemea mazao ya alizeti na nyanya.
Msangi naye aliumwagia sifa mradi wa MUVI kwa kusema kuwa umewajengea uwezo wajasiriamli ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha katika vikundi mbalimbali ili viweze kutambuliwa na wadau wenye malengo yanayoshabihiana na kukusanya nguvu za pamoja kumudu huduma na rasilimali zilizopo.
Amesema kuwa mradi huo utawaunganisha wajasiriamali wa zao la alizeti na wadau wapembejeo za kilimo pia utaibua ubunifu katika Nyanja za masoko, teknolojia na sera ili kuinua ufanisi katika minyororo ya thamani ya mazao ya alizeti na nyanya ambapo pia amesema majukwaa yasiishie katika ngazi ya mkoa pekee bali yaende pia hadi ngazi ya wilaya.
Aidha amesema wajasiriamali wakiwa kwenye vyama au vikundi wanakuwa na sauti inayoweza kusikika katika ushawishi na hivyo amewataka wajasiriamali kuunganisha nguvu zao pamoja ili waweze kuwa na uhusiano wenye tija kwa serikali na taasisi nyingine zilizopo katika ngazi za juu.
Katika hatua nyingine, Dumba aliwahimiza wanavikundi kutoka Njombe kufuata ushauri mzuri na mafunzo mbalimbali waliyoyapata kupitaia mradi wa MUVI unaolenga kuongeza thamani katika zao la alizeti na nyanya Njombe na Iringa.
Dumba ambaye pia amewahi kuwamtangazaji wa redio Tanzania, aliwahimiza wadau mbalimbali wa kilimo pamoja na halmashauri kuhakikisha zinashirikiana kwa pamoja na jukwa hili liloundwa kwa lengo lakuwezesha ushindani wa hali ya juu katika uzalishaji wa alizeti.
Mradi wa MUVI mkoani Iringa unafanya kazi chini ya Shirika la Viwanda Vidogovidogo (SIDO) na umejikita kuwainua wajasiriamali wa wadogo na wakati kwa kutilia msukumo mazao ya alizeti na nyanya.