Rea kutumia bil 100 kupeleka umeme vijijini


Baadhi ya wananchi wakipata maelezo kwenye banda la wakala wa usambazaji wa umeme vijijini (REA) kwenye maonesho ya Nishati na Madini Mnazi Mmoja.

Ismail Ngayonga na Salama Juma-Maelezo

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) imepanga kutumia kiasi cha sh bilioni 100 kwa ajili ya mradi wa usambazaji umeme katika mikoa 16 nchini.

Hayo yamebainishwa leo (jana) na Mkurugenzi wa huduma za ufundi wa REA, Mhandisi Bengiel Msofe katika maonyesho ya Wizara ya Nishati na Madini ya kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

Aliitaja mikoa itakayonufaika na mradi huo kuwa ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Mkoa wa Pwani-Kisarawe, Morogoro, Dodoma, SingidaMbeya, Rukwa, Tabora, na Kigoma.

Kwa mujibu wa Mhandisi Msofe Mikoa mingine itayofaidika ni pamoja na Kagera, Mwanza, Mara na Shinyanga, na kuongeza kuwa chini ya utekelezaji wa mradi huo wateja wote wanatarajia kuunganishiwa mita za luku.

Aidha aliongeza kuwa chini ya utekelezaji wa mradi huo jumla ya wilaya 41 katika mikoa iliyotajwa inatarajia kunufaika na mpango wa Serikali.

Akifafanua zaidi alisema kutokana na gharama kubwa zilizopo sasa za kuunganisha umeme majumbani, REA imepanga kuondoa ada ya kuunganisha umeme kwa wateja wake na hivyo kuwataka wananchi wa mikoa iliyotajwa kutandaza waya katika nyumba zao ili kuhakikisha kuwa malengo yaliyopangwa yanatekelezeka katika wakati uliopangwa.

Maonyesho hayo yaliyoanza juzi yalifunguliwa rasmi jana na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania Profesa Abdulkarim Mruma.