Mchungaji Mwasapile wa Loliondo anatibu Ukimwi!

Mchungaji Mwasapile wa Loliondo anatibu Ukimwi!
Mchungaji Ambilikile Mwasapile (kulia) akitoa dawa kwa wagonjwa wake.

Na Joachim Mushi

MCHUNGAJI mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapile, inasemekana amengundua dawa ya ajabu. Dawa hiyo anayodai inatibu magonjwa matano ameivumbua kwa  maelekezo aliyopewa na Mungu wakati akiwa ndotoni. 

Jina la dawa hiyo ni ‘mugarika’ na magonjwa yanayotajwa kutibiwa na dawa hiyo ni ugonjwa wa Kisukari, Shinikizo la damu, Kansa, Kifua Kikuu na Ukimwi.

Kwa mujibu wa maelezo ya mchungaji Mwasapile  anapohojiwa na vyombo vya habari anasema dawa yake inatokana na mmea aina ya mugarika ambao ni chakula kikubwa cha mnyama twiga unaopatikana porini.

Mchungaji anasema ameoteshwa miaka kadhaa iliyopita juu ya dawa hiyo, japokuwa imeanza kupata umaarufu siku za karibuni. Hata hivyo ndotoni aliambiwa atakapoanza kufanya kazi hiyo dunia itaamia kwake kwa mahitaji ya dawa hiyo.

Binafsi sina tatizo la dawa hiyo iliyojaa masharti kadhaa ambayo huenda yakawa magumu kwa watu wanaoitaji kusaidiwa ilhali wako mbali. Lakini hofu yangu ni uvumi huo na hali alivyo kwa sasa eneo la tukio.

Wananchi wengi ambao wanasumbuliwa na miongoni mwa magonjwa yanayotajwa kutibiwa na dawa hiyo wameanza kumiminika Loliondo, eneo analokaa mchungaji huyo ili kuweza kupata tiba.

Imani yao ni kwamba huenda dawa inayotajwa ikawa mwisho wa malazi yanayowakabili. Wagonjwa hao wanaenda kwa wingi kiasi kwamba tayari usalama wao u mashakani. 

Baadhi ya watu tayari wameanza kupoteza maisha kutokana na msongamano na foleni wakisubiri kupata huduma hiyo inayogharimu kiasi cha sh. 500 tu.  Huenda hali ikawa mbaya zaidi baadaye kwani magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza na kuangamiza wengi.

Kimsingi sipingani wala kuunga mkono ufanisi wa dawa hiyo kwa kuwa sina hakika kuwa inafanya kazi kiusahihi kama baadhi ya tetesi zilizopo. Huenda ikawa ndivyo au sivyo. 

Ukweli wa mambo ni kwamba lazima Serikali ijihakikishie kwa hilo na kuangalia usalama wa wananchi wake. Nasema hivyo hasa kwa kuzingatia Mwasapile ametaja pia kutibu ugonjwa hatari ambao inaaminika hadi leo hauna dawa.

Anasema anaweza kutibu Ukimwi na mgonjwa kupona baada ya muda mfupi tangu kunywa kikombe kimoja cha dawa yake. Huu ni mshtuko mkubwa na huenda ukawa ndiyo chazo cha kufurika kwa watu.

Lakini nabii huyu mstaafu si mtu wa kwanza kujitokeza na kudai anatibu Ukimwi, wapo wengi ambao wamekuwa wakiibuka na kutoa kauli kama hizo. Kama kauli hizi ni sawa na zile za waganga na manabii wengine ni kuwaibia wananchi. 

Kumuibia mtu si lazima utumie nguvu au kuchukua kitu pasipo idhini yake. Hata kitendo cha kutumia ulaghai wa njia ya kwamba unauwezo wa kufanya kitu, kumbe sivyo ni wizi.

Kwa mantiki hiyo Serikali inakila sababu ya kufuatilia suala hilo ili kubaini ukweli. Nasema hivyo kutokana na hali ya kutokuwa na usimamizi mzuri utapeli kama huo umekuwa ukitokea mara kadhaa.

 Mawasiliano: 0717030066, 0756469470, jomushi79@yahoo.com au joemushi.blogspot.com

Related Post

2 thoughts on “Mchungaji Mwasapile wa Loliondo anatibu Ukimwi!

  1. Asante Mushi kwa uchambuzi wako mzuri, na ninakubaliana na wewe kabisa kwamba dawa ya huyu Mwasapile inabidi ichunguzwe kabla ya wananchi kuibugia kwa fujo. Pamoja na hayo…je wewe una amini kwamba huyu Mwasapile ni Nabii? kwani umesema “Lakini nabii huyu mstaafu si mtu wa kwanza kujitokeza na kudai anatibu Ukimwi, wapo wengi ambao wamekuwa wakiibuka na kutoa kauli kama hizo”. Kama hauamini hivyo, basi neno “nabii” lilitakiwa liwe kwenye quotation…au sio? Pili huyu jamaa ni “Mchungaji” mstaafu na sio nabii mstaafu….Asante.

    1. uchambuzi wako Mushi uko makini.asante.lakini mi nasema ;ungekuwa na ndugu au mpendwa wako anayesumbuliwa sana kwa mda mrefu na magonjwa sugu yanayotajwa hapo juu, nafikiri ungetafuta kwanza tiba halafu tafakari baadae.MI NASHANGAA KUONA WANADAMU WANAVYOKUNA VICHWA KUTAKA KUELEWA INAKUWAJE MTI SUMU UNATIBU.YES, THIS IS HOW GOD CONFUSES WISES OF THIS WORLD.

      DONT YOU HAVE ALIVE TESTIMONIES FROM THOSE WHO HAVE BEEN SICK AND NOW HEALED BY GOD THROUGHOUT THIS DECOCTION?
      Nahisi, enzi zile za kisima cha siloe, walikuwepo watu wadadisi waliokufa na magonjwa yao wakitafakari kila siku; HIVI HUYU NI MUNGU KWELI ANAYEFANYA MAJI YATIBUKE, NA KWA NINI NI MTU MMOJA TU NDIO ANAPONA.MHMMM!HATA! HUYU SIO MUNGU…. MAANA ANGEKUWA MUNGU ANGESHUSHA UPONYAJI KWA WOTE WAGONJWA WANAOSUBIRIA KANDO YA KISIMA SILOE MIAKA NENDA RUDI.
      lakini je, haikuwa Mungu?

      Mi naona hekima, katika jambo hili la loliondo ni KUNYAMAZA KABISA kama Roho wa Mungu hajaongea na wewe maana waweza kumtenda Mungu dhambi kwa kumsemea mtumishi wako vibaya.BEWARE OF SLANDERING GODS’SERVANTS, ndugu!

      RENATUS

Comments are closed.