MABONDIA wa ngumi za Ridhaa wa Tanzania mwishoni mwa wiki iliyopita wamechezea kichapo baada ya kupigwa michezo minne kati ya mitano iliyochezwa na mabondia toka Zambia kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo.
Mapambano hayo ambayo yalikuwa ni ya kirafiki ya kimataifa kati ya nchi hizo mbili Tanzania na Zambia, yanayotambuliwa na Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Duniani (AIBA) yaliokuwa na raundi tatu kila mchezo ilishuhudia Said Hofu wa Tanzania akifungua pazia (kg 49) kwa kupigwa kwa pointi na Caristo Bwalia toka Zambia
Mpambano wa pili kg 56 ulishuhudia, Frank Nicolaus wa Tanzania akipigwa na Russel Mwamba wa Zambia kwa pointi pia. Kg 60 ndipo mtanzania Ismail Galiatano alimshushia ngumi nzito nzito John Chimpwele wa Zambia na kusababisha kuchanika juu ya jicho na kutokwa damu nyingi ndipo mwamuzi alisimamisha mchezo na kumpa ushindi Ismail Galiatano.(RSC)
Mpambano wa nne kg 64 Mtanzania Kassim Hussein alipokea kipigo toka kwa Charles Lumbwe kwa kupigwa kwa pointi. Funga kazi kg 75 ilivutia wengi maana Mohamed Chimbumbui wa Tanzania alipigwa kwa TKO na Mbachi Kaonga wa Zambia baada ya kumsukumizia makonde mazito na kushindwa kuyahimili na kujikuta akianguka kila mara.
Katibu wa Chama ngumi za ridhaa, Makore Mashaga alisema wamepoteza mpambano huo lakini anashukuru wamepata mazoezi ya kujiandaa na mashindano ya ndano yanayotarajiwa kuanza Novemba 26 kwenye uwanja wa ndani wa taifa, jijini Dar es Salaam. Mabondia watanzania walisema kupigwa kwao kunatokana na maandalizi hafifu waliyopata na mashindano kuahirishwa mara kwa mara pia kuliwafanya morali kushuka.
Naye Katibu wa Ngumi za Ridhaa wa Zambia Lut. Kanali Man Muchimba amesema amefurahi kucheza na watanzania kwani wamepata mazoezi ya kuwasaidia kucheza mashindano ya kanda ya tano yatakayofanyika nchini kwao mapema Desemba.