











CHAMA cha Kusimamia Haki Miliki kwa Wasanii na Kazi za Sanaa (COSOTA) kimekutanisha wanachama wake na wadau wengine kisha kutoa semina juu ya namna bora ya kusimamia kazi zao ili ziwafaidishe zaidi kuliko wanavyofanya baadhi ya wasanii ambapo hujikuta kazi zao zinawanufaisha wengine.
Miongoni mwa mada ambazo zilitolewa kwa wanachama wa COSOTA pamoja na wadau mbalimbali ni namna ya kulinda haki za wasanii katika mazingira ya ulimwengu wa dijitali, namna sahihi ya kusimamia haki ya kazi za wasanii, ufafanuzi juu ya mikataba mbalimbali inayosimamia haki miliki pamoja na ulindaji wa haki miliki kwenye filamu.
Katika semina hiyo washiriki pia walielezwa juu ya umuhimu wa kusajili kazi zao na kampuni zinazosimamia kazi hizo pamoja na namna bora ya kuandaa mkataba kwa kuzingatia maslahi ya muhusika. Burudani mbalimbali zilitolewa katika semina hiyo iliyofanyika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam na kufunguliwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Bi. Janeth Mbene.
