Serikali yatangaza rasmi mikoa mipya minne na wilaya 19

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda

Na Mwandishi Maalumu

SERIKALI imetoa matangazo rasmi ya Serikali (Government Notices) kuhusu uanzishaji wa mikoa mipya minne na wilaya mpya 19 ambayo yamechapishwa tangu Machi 2, mwaka huu. Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema matangazo hayo yalisainiwa na Rais Jakaya Kikwete Machi Mosi, 2012. Alisema mikoa mipya kwamujibu wa taarifa hiyo ni Geita, Katavi, Njombe na Simiyu. Mikoa hii tayari imechapishwa katika Tangazo la Serikali Na. 72.

Alisema Wilaya 19 ambazo zimeanzishwa na kuchapishwa katika Tangazo la Serikali Na.73 ni Buhigwe, Busega, Butiama, Chemba, Gairo, Ikungi na Itilima. Wilaya nyingine ni Kakonko, Kalambo, Kaliua, Kyerwa, Mbogwe, Mkalama na Mlele. Nyingine ni Momba, Nyang’hwale, Nyasa, Uvinza na Wanging’ombe.

Kwa mujibu wa matangazo hayo makao makuu ya mikoa hiyo mipya minne yatakuwa kama ifuatavyo: Geita (Geita), Simiyu (Bariadi) Njombe (Njombe) na Katavi (Mpanda). Mikoa hiyo itakuwa na wilaya zifuatazo; Geita utakuwa na wilaya tano za Bukombe, Chato, Geita, Mbongwe na Nyang’hwale. Mkoa wa Katavi utakuwa na wilaya mbili za Mlele na Mpanda. Mkoa wa Njombe utakuwa na wilaya nne za Makete, Njombe, Ludewa na Wanging’ombe wakati mkoa wa Simiyu utakuwa na wilaya tano za Bariadi, Busega, Maswa, Meatu na Itilima.

Aidha alisema makao makuu ya wilaya mpya zilizoanzishwa ni kama ifuatavyo: Buhigwe (Buhigwe); Busega (Nyashimo); Butiama (Butiama); Chemba (Chemba); Gairo (Gairo); Ikungi (Ikungi) Itilima (Lagangabilili); Kakonko (Kakonko); Kalambo (Matai) na Kaliua (Kaliua).

Nyingine ni Kyerwa (Rubwera); Mbogwe (Mbogwe); Mkalama (Nduguti); Mlele (Inyonga); Momba (Chitete); Nyang’hwale (Kharumwa); Nyasa (Mbamba Bay); Uvinza (Lugufu) na Igwachanya (Wanging’ombe).

Julai 2010, kabla Rais Kikwete hajatoa hotuba ya kulivunja Bunge, Serikali ilitoa uamuzi wa kuunda mikoa mipya minne na wilaya mpya 21. Hata hivyo, baada ya kuhakiki mipaka ya maeneo hayo yote na kuandaa maelezo ya mipaka hiyo vizuri (boundary descriptions), wilaya zilipunguzwa na kubakia 19.

Related Post

2 thoughts on “Serikali yatangaza rasmi mikoa mipya minne na wilaya 19

  1. Ukifuatilia kwa MAKINI utagundua kuwa hatimaye kila kabila limepata wilaya yake!…kitakachofuata ni kila kilahaja cha kabila kupata tarafa yake!…utawala wa kikabila umeota mizizi!….sera hii ni kama ile ya wajerumani ya ”GAWANYA UTAWALE”

  2. …INABIDI KUYAUNGANISHA MAKABILA MENGI ILI WATU WA MAKABILA MBALIMBALI WAUNGANISHE VIPAJI VYAO NA UWEZO WAO KUJILETEA MAENDELEO,VINGINEVYO TUNAJENGA TANZANIA AMBAYO HAITAJENGEKA BADALA YAKE ITADUMAA!!…USHAURI WANGU KWA WATAWALA NA CHAMA TAWALA CCM NI KUACHANA NA SERA HII YA KIKABILA NA KUJARIBU KUKAA NA VYAMA VINGINE HASA CHADEMA NA KUJIFUNZA MAONO YA CHADEMA KUHUSU SERA YA MAJIMBO AMBAYO IMELENGA KUYAUNGANISHA MAKABILA MENGI KWA PAMOJA NA KUFANYA KAZI KAMA KUNDI MOJA LENYE LENGO MOJA….TANZANIA YA SASA HAIHITAJI KILA KABILA KUJITAWALA BALI KUUNGANISHA NGUVU NA VIPAJI VYA MAKABILA MBALIMBALI KUJENGA UCHUMI NA MAENDELEO MENGINE….CCM IJADILIANE NA CHADEMA KATIKA HILI KWANI WAKIKIMBILIA KUIGA BILA ”CONSULTATION” WATAISHIA KUFANYA KAMA LILIVYO SWALA LA KATIBA MPYA NA UJENZI WA VYUO VIKUU MKOANI DODOMA KAMA AMBAVYO CHADEMA WALIJINADI MWAKA 1995,2000, NA 2005 NA HATIMAYE CCM IKAIGA NA KUTEKELEZA BILA MAONO YA KITAIFA ZAIDI NA KUWEKA MAONO YA KI-CCM!

Comments are closed.