Odinga Ayapinga Matokeo ya Urais Yanayoendelea Kutangazwa Kenya

Mgombea nafasi ya urais, Raila Odinga akipiga kura.

 

MGOMBEA urais wa muungano wa upinzani nchini Kenya National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga amepinga matokeo ambayo yanaendelea kutangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo, IEBC. Raila Odinga ametoa kauli hiyo usiku wa kuamkia leo akizungumza na wanahabari.

Bw Odinga amesema tume hiyo imekuwa ikitangaza matokeo kwenye tovuti yake bila kufuata utaratibu unaofaa. Aliongeza kuwa kabla ya matokeo yoyote kutangazwa, IEBC inafaa kuwapa maajenti wa vyama Fomu 34A kutoka vituoni. Alisema kwa sasa, bila kuwepo kwa fomu hizo, ni vigumu kubaini matokeo yanayopeperushwa yanatoka wapi.

“Mfumo umeacha kufanya kazi. Sasa ni mitambo inayopiga kura. IEBC wamesema kwamba hakuna chama chochote kilichopinga matokeo. Lakini vyama vitapingaje matokeo bila kujua asili yake? Ni fomu 34A pekee zinazoonesha chanzo cha matokeo.” Kwa hivyo, tunakataa matokeo yote yaliyotangazwa kwa sasa na kuitaka tume ya IEBC itoe fomu 34A za kila kituo kabla ya matokeo zaidi kutangazwa.”

IEBC imekuwa ikitangaza matokeo ya urais mtandaoni, na kufikia saa tisa na robo alfajiri, matokeo hayo yalikuwa yanamuonyesha Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee akiwa mbele na kura 6331140 (55.27%) naye Bw Odinga akiwa na kura 5031737 (43.92%). Matokeo hayo ni ya kutoka vituo 295319 kati ya vituo 40883 nchini humo.

“Hii ni kompyuta inayopiga kura,” alisema Bw Odinga akikataa matokeo hayo. Hali ya wasiwasi imekuwa ikitanda katika kituo cha taifa cha kujumlishia na kutangaza matokeo katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi. Matokeo yalianza kutiririka baadaye Jumanne jioni baada ya shughuli ya kuhesabiwa kura kuanza. Matokeo hayo yamekuwa yakionesha Bw Kenyatta akiongoza.

Wakati huo huo, Katibu mkuu wa chama cha Jubilee chake Rais Uhuru Kenyatta, Bw Raphael Tuju, ameambia wanahabari kwamba madai ya muungano wa upinzani Nasa kwamba matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi IEBC hayaeleweki si ya kweli. Bw Tuju amesema upinzani unafaa kukubali kwamba haukufanya vyema katika uchaguzi uliofanyika Jumanne.

Amesema katika kaunti zote ambazo Bw Kenyatta alishinda mwaka 2013, hakuna kaunti hata moja ambayo ameipoteza kwa upinzani. Badala yake, amesema chama hicho kilifanikiwa kupata uungwaji mkono maeneo ambayo hakikufanya vyema uchaguzi uliopita mfano Nyamira na Kisii, wakati huu Jubilee walifanya vyema. Upinzani ulikuwa umelalamika kwamba IEBC imekataa kutoa Fomu 34A za kuthibitisha matokeo ya urais kutoka vituo vya kupigia kura.